Bwana Remigius Halala, Mthibiti ubora wa shule Wilaya ya Igunga, amewataka maafisa elimu Kata kufuata hatua nne za mzunguko wa Mafunzo endelevu ya kukuza taaluma, wakati alipokuwa akifungua mafunzo endelevu ya Maafisa Elimu Kata katika ukumbi wa Maxwell majuzi tarehe 10.05.2018.
“ Lengo la Mafunzo endelevu ni kukuza taaluma kwa Maafisa Elimu Kata, kuinua kiwango cha utendaji kazi cha Maafisa Elimu kata nchini kote kwa kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuhakikisha kuna utoaji elimu bora kwenye shule za awali, msingi na sekondari” aliiongeza Bwana Remigius Halala.
Hatua hizo nne muhimu alizitaja kuwa ni kutengeneza mpango binafsi wa kujifunza, kujaza fomu ya maombi, kukubali kujisajili na mafunzo na kujaza fomu ya maendeleo ya mafunzo endelevu
Bwana Remigius Halala, aliendelea kuwafafanulia baadhi ya sifa zinazozingatiwa katika uteuzi wa Maaafisa Elimu Kata, kwa sasa kuwa ni angalau mwenye shahada ya kwanza, awe amepata mafunzo kwenye chuo kinachotambuliwa,na mwenye uzoefu usiopungua miaka mitano, mwenye utayari wa kusimamia na kutekeleza Sera ya elimu kikamilifu, mwenye uwezo wa kuwasiliana kikamilifukatika lugha ya Kiswahili na Kiingereza katika kuongea na kuandika, mwenye uwezo wa kina kuhusu eneo analolifanyia kazi na mwenye mwenendo mzuri kitabia na anayeheshimika kwa wanajamii wote.
Naye Afisa Elimu Taaluma Wilaya ya Igunga, Bwana Edgar Kulwa, aliwasisitizia Maafisa Elimu kata kubadilika kulingana na maendeleo ya TEHAMA kwani taalum, yao itaonekana bora pale watakapojipambanua na kujiendeleza kwa kujisomea, kwani utaalam wa TEHAMA utawasaidia kwenye shughuli nyingi za maendeleo ya kitaaluma na kiuchumi.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa