Walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wamepongezwa kwa kuongeza kiwango cha ufaulu katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba na kidato cha nne mwaka jana(2016). Ambapo matokeo ya kidato cha nne yamepanda kutoka 79% ya mwaka 2015 hadi 82% mwaka 2016; hivyo kuifanya halmashauri kushika nafasi ya 9 kitaifa. Hali kadhalika kwa upande wa shule za msingi kiwango cha ufaulu kimepanda kutoka 42% ya mwaka 2015 hadi 68% mwaka 2016.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Peter Onesmo Maloda kwa niaba ya Waheshimiwa madiwani wakati wa kikao cha Baraza la madiwani cha tarehe 12 Mei, 2017 katika Ukumbi wa mkutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.
Aliwataka walimu wakuu na wakuu wa shule wote kuhakikisha wanaimarisha mikakati iliyopo ili waweze kupata matokeo mazuri zaidi kwa kipindi cha mwaka 2017 na kuwataka kuendelea kujituma.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika sekta ya Elimu, Mwenyekiti aliendelea kuwasisitiza walimu wote Wilayani kudumisha umoja na umilivu, kwani uongozi wa Halmashauri unatambua uwepo wa changamoto husika na unaendelea kuzifanyia kazi.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa