BARAZA la Madiwani wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora limewapongeza Wataalam wa Halmashauri hiyo kwa kuandaa vema Rasimu ya Bajeti ambayo inayodaiwa kuwagusa wananchi pindi itakapoanza kutekelezwa.
Pongezi hizo alizitoa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo jana, Lucas Bugoto wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichokaa kwa lengo la kujadili na kupitisha Bajeti ya mwaka wa fedha 2025 hadi 2026 yenye jumla ya Sh. Bilioni 53.
‘’Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya hakika ninawapongeza Watalamu na Madiwani bajeti hii iliandaliwa na imechakatwa kisayansi hali ambayo imesababisha kupita kwenye Kamati zote bila ya kupingwa,’’ alisema Bugota.
Alieleza kuwa imezingatia vipaombele vya kwenda kwasaidia wananchi ukilinganisha na bajeti ambayo wanaitekeleza hivi sasa kwa sababu wamekua wakipeleka asilimia 40 kila mwaka kwa asailimia 100.
‘’Bajeti yetu inakua haina kelele kwa sababu tunatekeleza na tunamsaidia Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambae amekua analeta fedha nyingi na kila kijiji na kata kunamradi na sisi Halmashauri ni jukumu letu kuitenga asilimia 40 na kuipekeleka kwa asilimia 100 kuunga mkono juhudi za serikali,’’ alisema.
Akizungumza katika Baraza hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sauda Mtondoo aliwaagiza Madiwani na Wataalamu hao kuendelea kuhakikisha wanafunzi ambao hawajaripoti shule waripoti kabla ya serikali haijanza kuchukua hatua za kuwakamata wazazi na walezi.
Alisema mwiitikio bado ni mdogo kwa sababu takwimu zinaeleza kuwa kidato cha kwanza ni asilimia 62, darasa lakwanza ni asilimia 83 na darasa la awali asilimia 50.
‘’Ndugu viongozi tukahamasishe wazazi wawepeleke watoto shuleni, tunataka ifikapo tarehe 28 mwezi huu watoto wote wanaostahili kuwa shule wawe shule vinginevyo tarehe moja mwezi Machi tutaanza oparesheni na wale ambao hawatakua wametekeleza wito huo tutawachukulia hatua,’’ alisisitiza DC Sauda.
Kaimu Mgurugenzi wa Halmashauri hiyo, Joseph Mafuru alisema wanapokea ushauri na maelekezo yaliotolewa katika kikao hicho na kuahidi wataboresha bajeti hiyo ambayo itatatua changamoto zilizoko kwa wananchi.
Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi wa wilaya hiyo, Shahibu Dadi aliahidi kuwa wameweka katika bajeti hiyo ununuzi wa Vishikwambi ambavyo vitafanikisha kuendesha vikao kidijitali kwa mwaka wa fedha ujao.
‘’Mheshimiwa Mwenyekiti nilihakikishie baraza hili kuwa bajeti ya Vishikwambi imezingatiwa,’’alithibitisha.
Naye Katibu wa Madiwani ambae ni Diwani wa Kata ya Bukoko, Jidashema Mwandu aliahidi kuhakikisha wanafunzi wote wanakwenda shule bila ya kusukumwa au kukamatwa kwa wazazi na walezi wao.
Rasimu yabajeti imepitishwa ikiwa na vipaombele vya kuimarisha shughuli za utawala bora, mafunzo kwa watumishi, kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya, kuimarisha usafi wa mazingira, kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari, kuwezesha wananchi kiuchumi, kupima na kumilikisha maeneo ya umma na kuimarisha uzalishaji wa pamba.
==== //// ==== //// =====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa