MKURUNGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Selwa Abdalla Hamid amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Watumishi wengi wa kada ya afya hususan katika kipindi hichi ambacho Igunga inakua kwa kasi na vituo vya afya na zahanati zimejengwa za kutosha.
Selwa ametoa shukran hizo wakati akiongea na Watumishi wa Kada hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Wilaya hiyo.
‘’Hakika kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa Watumishi wengi kwa sababu tulikua na uhitaji mkubwa hususan kwenye huduma za afya,’’ alisema.
Aidha, aliwataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa weledi wakizingatia miiko ya taaluma zao, kuepuka kuomba rushwa kwa wagonjwa, kutotumia lugha mbaya kwa wagonjwa ikiwemo kuingia kazini huku wakiwa katika hali ya ulevi.
Pia, aliwahakikishia kuwa Halmashauri itaendelea kuwathamini na kuwawezesha kupata stahiki zao kulingana na miongozo ya serikali.
‘’Ndugu zangu niendelee kuwakumbusha kuwa Halmashauri haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtumishi yoyote atakaeonesha utovu wa nidhamu,’’ alikemea.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa wilaya hiyo, Hamis Hamis alisema Serikali imeboresha mifumo mbalimbali ya watumishi.
‘’Niwakumbushe Watumishi wenzangu tuitumie hii mifumo kwa sababu inatusaidia kugundua mapema kama kuna taarifa hazipo sahihi, hivyo kumtaarifu Mkurugenzi kwa barua kwa lengo la kuhakikisha taarifa zinakua sahihi,’’ alisema.
Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Lucia Kafumu alisema katika wilaya hiyo walipangiwa watumishi 63 ambapo watumishi 61 walikwisha ripoti na wapo kwenye vituo wakiendelea kuwahumumia wananchi.
Akizungumzia kituo cha Afya Nanga ambacho baadhi ya majengo yake yamejengwa kwa fedha za Halmashauri hiyo milioni 400, Lucia aliweka wazi kuwa wamepeleka Daktari mmoja na Mtu wa Usingizi kwa lengo la kuanza kutoa huduma za upasuaji hivi karibuni.
Naye Afisa Muuguzi na Mtaalam wa Dawa za Usingizi na Ganzi wa Hospitali hiyo, Daud Mahenge alisema wamekubali kubadilika na kuendelea kuwa waadilifu katika kazi zao.
==== //// ==== ///// =====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa