WANANCHI wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora wako mbioni kunufaika na Mradi wa Umwagiliaji Mwamapuli utakaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Benki hiyo imetenga takribani Dola milioni 300 ambapo milioni 70 zitapelekwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutekeleza Skimu 23 huku mradi wa Mwamapuli ukitengewa Dola milioni 1.3 sawa na sh. Bilioni nne za kitanzania.
Akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NRC), Salome Mallamia, Mkurungezi Mtenjaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani hapa, Bi. Selwa Abdalla Hamid amemuahidi kiongozi huyo kuzifanyia kazi changamoto zozote zitakazodaiwa kukwamisha Mradi huo.
Alisema wanayo nafasi ya kuendelea kukaa na wakulima kwa lengo la kuwapa elimu ikiwemo kuwashirikisha viongozi wa ngazi tofauti ikiwemo watendaji wa kata na kijiji.
Aliweka wazi kuwa Igunga kwa kiwango kikubwa inategemea mapato kwenye kilimo, hivyo kwa lengo la kuendelea kukuza mapato watajikita kwenye kilimo licha yakua baadhi ya mapato yanapatikana katika madini ya dhahabu.
‘’Ninaamini kilimo kinaweza kuendelea kuwanyanyua watu wetu, ni jukumu langu kuhakikisha maslahi na mapato ya wananchi na Halmashauri yanapanda’’ alisema na kuahidi kuwa:
‘’Mtapata mabadiliko chanya kwa lengo la kuhakikisha wakati mnaendelea msipate shida yoyote kuhusu kuwekeza na kuleta miradi ikiwemo kutoa sifa nzuri kuwa Igunga imejipanga,’’ alisema.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NRC), Salome Mallamia alimuomba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuifanyia kazi changamoto ya uharibufu wa miundombinu ambayo inadaiwa kuharibiwa kutokana na uingizaji wa N’gombe zinazofuata malisho.
==== //// ==== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa