MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora, Bi. Selwa Abdalla Hamid amewapongeza Venyeviti wa Vijiji na Vitongoji walioshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024.
Bi. Selwa ametoa pongezi hizo wakati wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo wenyeviti hao wakiwemo Watendaji wa Vijiji na Kata yaliofanyika Jumamosi Mei 10, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Maxwel mjini hapa.
Amewakumbusha wadhifa na madaraka waliopewa ni lazima wasimamie vema kwa lengo la kuhakikisha wanatimiza majukumu yao huku akiwaasa wanapokwama kutosita kurejea kwa viongozi wao kupata msaada.
‘’Ndugu zangu mimi Mkurugenzi wenu nitakua bega kwa bega kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanaendelea kuwafikia wananchi katika maeneo yao,’’ amesisitiza na kutoa wito:
‘’Nendeni mkalete mabadilko chanya ya kimaendeleo ikiwemo kusimamia miradi iliyopo katika maeneo yenu na kutoa taarifa mahali sahihi.’’
Katika hatua nyingi, Bi. Selwa amewasisitiza nidhamu ya fedha hususani zile za serikali kwa sababu zinamiongozo yake, hivyo wadumishe uadilifu na kuambatana na burasa na hekima wakati wanapotoa maamuzi bila ya kuvunja sheria, taratibu na kanuni.
Kwa upande wa Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa, Scholastica Nyabweke ameeleza viongozi hao wako karibu na wananchi, hivyo wanaowajibu wa kuhakikisha miradi shirikishi ya maendeleo inasimamiwa ipasavyo kwa sababu serikali imekua ikitoa fedha nyingi.
Ameongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuendelea kuhakikisha wananchi wa Igunga wananufaika na maendeleo, hivyo wakayatumie mafunzo haya kwa lengo la kuleta tija.
Naye Mwenyeketi wa Kijiji cha Isakamaliwa, Ntelezu Itinga ameshauri mamlaka husika kuwapatia nakala za mafunzo hayo kwa lengo la kuendelea kujikumbusha na kuwa na weledi kujiepusha na makosa.
Mafunzo hayo yamehusisha mada ya Sheria za Uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Muundo, Majukumu na Madaraka ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji, Uongozi na Utawala Bora, Uendeshaji wa Vikao na Mikutano katika Ngazi za Vijiji Mitaa na Vitongoji.
Aidha, mada zingine ni Uibuaji, Upangaji na Usimamizi wa Miradi Shirikishi ya Kijamii, Usimamizi wa Ununuzi, Usimamizi wa Ardhi na Udhibiti wa Uendeshaji Miji na Masuala Mtambuka.
==== //// ==== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa