MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Bi. Selwa Abdalla Hamid amewaasa Watumishi wanaokwenda kushiriki michezo iliyoandaliwa na Shirikisho la Michezo Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) kufanya vema na kurudi na ushindi.
Aidha, amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaongezea bajeti jambo ambalo limepelekea yeye kuiwezesha timu ya Halmashauri kushiriki michezo hiyo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hiyo.
Akizungumza na Watumishi hao, leo Alhamisi Agosti 14, 2025, katika Ofisi ya Halmashauri hiyo, Bi. Selwa amesema ni wajibu kuendelea kumshukuru Mhe. Rais Dk. Samia kwa kuwawezesha bajeti iliyofanikisha jambo hili ambalo ni kwa mara yakwanza kushiriki tangu Halmashauri hiyo ilivyoanzishwa 1994.
‘’Ninafurahi mtakavyopepeprusha bendera ya Igunga huko jijini Tanga, hivyo jambo la msingi ni kushiriki vema hivyo jisikieni fahari na mkacheze kwa bidii,’’ amesema na kuongeza kuwa:
‘’Niwaombe mwende huko kama familia moja na kitu kimoja huku mkitanguliza mbele nidhamu na heshima.’’
Amewataka kuheshimiana wao kwa wao na wale watakaokutana nao katika mashindano hayo huku akiwaasa kutoweka dosari ya jina la Halmashauri yao.
‘’Ninafurahi! leo mpo wachache lakini mwakani tutajitahidi bajeti iongezeke zaidi twende wengi kwa sababu michezo ni afya na nia ajira,’’ ameahidi.
Kwa upande wa Ofisa Michezo wa Halmashauri hiyo, Fadhili Kayange amemshukuru na kumpongeza Mkurugenzi huyo kwa kufanikisha jambo hilo kwa sababu ameandika historia mpya ya Halmashauri hiyo.
Naye Ofisa Utumishi wa Halmashauri Hiyo, Rahel Hagai amemuahidi Mkurugenzi huyo wataitambulisha vema Halmashauri hiyo.
‘’Tunakushukuru Mkurugenzi wetu Bi. Selwa Abdalla Hamid hakika kutupa kibali na kutugharamikia ni jambo kubwa, tunasema asante sana!” ameshukuru Rahel.
========== ///////// ==========
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa