MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Mhe. Shabani Hemedi ameliongoza Baraza la Madiwani kumpongeza Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuiletea fedha nyingi zinazotekeleza miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Mhe. Hemedi ametoa pongezi hizo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2025 hadi 2026 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo mjini Igunga januari 28, 2026.
Ameliomba Baraza hilo kutowavumilia watumishi watakaoshindwa kusimamia miradi iliyoletewa fedha na Rais Dk. Samia kusimamia miradi ikamilike kwa wakati.
"Waheshimiwa Madiwani itakapofika hatua hiyo, niwaombe mniunge mkono, mtumishi wa namna hiyo hatakua na sifa ya kufanya kazi katika Halmashauri hii," amesisitiza.
Akizungumzia Vishikwambi alivyogawa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Selwa Hamid, Mhe
Hemedi amempongeza Mkurugenzi huyo huku akiwataka Madiwani wakavitunze vishikwambi.
Aidha, amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa kumuunga mkono Mhe. Rais Dk. Samia ambae ameadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda mti jambo ambalo linatoa tafsiri yakutokata miti kutengenezea karatasi.
Katika hatua nyingine, amewahimiza Madiwani kuwahamasisha wazazi na walezi katika kata zao kuhakikisha watoto na wanafunzi wanaotakiwa kuwa shule wanapelekwa shule kwa sababu muda ndio huu.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Selwa Hamid amesema ametimiza ahadi ya kugawa vishikwambi kwa Madiwani 46 kwa lengo la kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia kuhusu matumizi ya kidijitali.
"Leo tunaungana na Mhe. Rais Dk. Samia katika matumizi ya kidijitali, hivyo tunaanza kutumia vishikwambi katika vikao vyetu na kuepukana na matumizi ya karatasi," amesema.
Aidha, amesena wamepokea maelekezo yote na watayafanyia kazi.
Naye Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Halmashauri hiyo, Ndug. Hamisi Hamisi amewaomba viongozi hao kuvitunza vishikwambi hivyo kwa sababu ni mali ya serikali.
================

Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa