MRAKIBU Mwandamizi wa Jeshi la Magereza wa Wilaya ya Igunga mkaoni Tabora, Kaganyero Kegori amewaongoza askari wa jeshi hilo kuchangia damu zaidi ya chupa 13 katika Hospitali ya wilaya hiyo.
Mrakibu Kegori amefanya zoezi hilo Jumamosi Agosti 23, 2025 katika Hospitali ya wilaya hiyo mjini hapa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jeshi hilo kutimiza miaka 64 baada ya uhuru wa nchi hii.
‘’Sisi ni sehemu ya jamii tunachangia damu kwa lengo la kuendelea kuokoa baadhi ya wananchi ambao wanauhitaji wa Damu,” amesema.
Akizungumza baada ya tukio hilo Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Jesto Maguzu amelishukuru jeshi hilo kwa namna ambavyo wamejitoa kufanya usafi na kuchangia damu.
‘’Hakika tunalipongeza jeshi la Magereza kwa kutumia muda wao kuja kufanya usafi na kuchangia damu, tunaomba Taasisi nyingine zijitokeze kuchangia damu kwa sababu uhitaji bado upo,’’ amesema na kuongeza kuwa:
‘’Hospitali yetu ipo karibu na barabara kuu ambapo ajali zinaweza kutokea na changamoto nyingine zinazohitaji damu.’’
Aidha, amesema wamepata zaidi ya chupa 13 za damu ambazo zitaendelea kuwasaidia wananchi ambao wanahitaji.
Kwa upande wa mmoja wa wananchi wanaoishi wilayani hapa, Scholastica Amos amelipongeza na kulishukuru jeshi hilo kwa kujali maisha ya watu wanaohitaji damu huku akitoa wito kwa jamii iendelee kuchangia damu kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji.
Ameeleza wanaamini damu iliyopatikana itaendelea kuokoa maisha ya Mama Wajawazito na Watoto.
Askari wa Jeshi la Magereza wamefanya usafi na kuchangia damu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya jeshi hilo ya miaka 64 ya kuanzishwa kwake.
=========
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa