MKUU wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora,Mhe. Sauda Mtondoo amewashukuru Wajumbe wa Kamati ya Lishe Wilaya kwa kuja na bajeti ambayo italeta matokeo chanya kwenye afya za wananchi.
Mhe. DC Sauda ametoa shukrani hizo Jumatatu Disemba 23, 2024 wakati wa kikao cha Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Kamati hiyo kwa mwaka wa fedha 2025 hadi 2026 kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.
Alisisitiza kuwa bajeti walioipanga ikatoe matokea chanya kwa jamii kwa lengo la kupunguza utapiamlo, magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe.
‘’Fedha hii iliyotengwa ni nyingi, hivyo hatuwezi kuzungumzia uchumi au maendeleeo kama afya zetu haziko vizuri, afya inaanzia kwenye lishe,’’ alisema DC Sauda na kuongeza kuwa:
‘’Mtu akiwa na lishe bora hata magonjwa ya hovyo hovyo yanamuepuka, hivyo tunatamani iwe jamii yenye lishe bora kwa lengo la kuhakikisha inaepukana na magonjwa na kujikita katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.’’
Alisema hatua hiyo itasaidia kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo wataalamu wawe na ubinifu utakaoleta matokeo chanya.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Joseph Mafuru aliwashauri Wakuu wa Idara za Elimu kuyatumia maeneo ambayo yapo karibu na shule yalimwe kwa lengo la kuhakikisha chakula kinapatika na wananfunzi wanakula na kunywa uji pindi wawapo shuleni.
Naye Mkuu wa Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Lucia Kafumu aliwashauri Maafisa Lishe kuwa na ubunifu wa kuanzisha bustani ya lishe, kuuza maziwa na kufuga kuku.
‘’Tuendelee kuboresha mpango wetu kwa lengo la kuhakikisha unajibu changamoto kwenye mambo ya lishe,’’ amesisitiza.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa