MKUU wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Mhe. Sauda Mtondoo amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupambana kuhakikisha mambo yanayowagusa Watanzania wakiwemo wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) anatafuta fedha kwa lengo la kuhakikisha mpango huo unaendelea.
Mhe. Sauda ametoa shukran na pongezi hizo Ijumaa Januari 31, 2025 wakati akiongea na Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kijiji cha Igumila Kata ya Ziba wilayani hapa.
Aidha, aliweka wazi kuwa dhamira ya serikali ni kuona Wananchi wanainuka kutoka walipokua na kupiga hatua zaidi, hivyo wajitafakari na kuuchukia umaskini kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakipokea fedha kwa muda mrefu.
‘’Ndugu zangu hichi kiasi kidogo mnachokipata endeleeni kuweka mikakati ya kuhakikisha mnaondokana na umaskini, ninawaomba msimame imara kwa lengo la kutoka katika hali ya umaskini kwa sababu inawezekana,’’ alisistiza.
Alifafanua kuwa serikali inaendelea kuwajali, hivyo wanaweza kulima na kupata mazao ambayo wanaweza kuyatumia kwa chakula na mengine kuuza, kufuga kuku au mbuzi kisha wakawavuna na kuwauza kwa lengo la kujiongezea kipato.
Alisema ni lazima wawe na dhamira ya dhati ya kuuchukia umaskini kwa kuanzisha hata biashara ndogondogo ambapo wataweza kuendelea.
‘’ Ninawahamasisha ndugu nzangu kuuondoa umaskini licha yakuwa sio rahisi lakini inahitaji moyo na ujasiri na kujituma,’’ alisema.
Kwa upande wa Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Elizabeth Rwegasira aliwataka wasimamizi wa miradi inayotekelezwa kupitia mpango huo kuongeza usimamizi wa karibu kwenye miradi hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanapata matokeo ya kudumu.
Awali akiwasilisha taarifa fupi mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya kwa niaba ya Wanufaika wa TASAF Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Igumila, Jackrine Gibe alisema kijiji hicho kinatekeleza afua ya Uhawilishaji wa Fedha (CCT) na Miradi ya Ajira za Muda (PWP).
Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024 hadi 2025 walipokea fedha sh. milioni 15.072 kwa walengwa 144 hivyo kufanikiwa kujikwamua kutoka kwenye hali ya umaskini uliokithiri.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa