MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Mhe. Shabani Hemedi amewashukuru na kuwapongeza wakufunzi kwa kuwaelimisha mambo mengi kuhusu kuendesha Halmashauri kwa tija.
Mhe. Shabani ametoa shukran na pongezi hizo leo, Ijumaa Januari 23, 2026 wakati wakuhitimisha mafunzo kutoka kwa wakufunzi wa TAMISEMI na Hombolo tawi la Shinyanga yaliyofanyika katika ukumibi wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
Kwa upande wa Meneja Rasilimaliwatu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Kampasi ya Shinyanga, Michael Boniface amewaomba Madiwani na Wataalamu hao, kuelewa Wataalam wa Chuo hicho wapo tayari kuendelea kutoa mafunzo bure inapohitajika kwa sababu ndio maelekezo ya Mkuu wa Chuo hicho.
Aidha, ameongeza kuwa wanapokua na Watumishi ajira mpya na hawajapata mafunzo elekezi (orientation) wawape mwaliko watakuja kutoa mafunzo hayo.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa watumishi hao kujiandaa kustafu tangu siku ya kwanza walioanza kazi kwa kuanza kujenga kidogo kidogo kwa lengo la kujiepusha kushangaa wakati wa kustafu unapofika.
"Nidhamu ya kazi ni msingi wa mafanikio mema kazini, viongozi na wafanya kazi lazima wote tuwe na nidhamu, migogoro na migongano ya kazini ni ukosefu wa nidhamu," amesisitiza.
Kwa upande wa Mkufunzi kutoka Chuo hicho katika tawi hilo, Lenatha Mwangesi amewaeleza Madiwani ni wajibu wao kutumia ujuzi na vipawa vyao kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa lengo la kuhakikisha mipango mingi ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo inatimia.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Diwani wa Kata ya Isakamaliwa, Maganga Daud amewaomba wakufunzi hao kulifikisha kwa viongozi wa kitaifa kuhusu posho za Madiwani ziongezeke huku akiwaomba wabunge wawatetee bungeni na lisiwe swala la mchakato kwa sababu limekua la muda mrefu.
================////////////////




Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa