TIMU ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, imefanya ziara fupi Jijini Mwanza kwa lengo la kufanya utalii mdogo wa ndani huku ikifanya tathimini ya utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali ikiwemo kusimamia kwa ufanisi mkubwa miradi ya maendeleo inayoendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Timu hiyo imefanya tathmini yake hivi karibuni baada ya kufanya vyema katika kila sekta mbalimbali ndani ya mwaka wa fedha 2024/2025 huku ikiahidi na kuweka mikakati thabiti na imara ya kuendelea kufanya kazi zake kwa bidii na uweledi mkubwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri hiyo, Bi. Selwa Abdalla Hamid amewashukuru na kuwapongeza viongozi hao kwa kuendelea kuipaisha Igunga.
Amedokeza kwa upande wa Fedha na Uhasibu, Halmashauri hiyo imepata hati safi mfululizo kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 huku ikikusanya mapato na kuvuka lengo kwa asilimia zaidi ya 103 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na 2024/2025.
Aidha, akizungumzia kuhusu miradi, Bi. Selwa amewaka wazi katika mwaka huo wilaya hiyo ilipokea takribani sh. 115.5 bilioni kutekeleza miradi ya maendeleo.
"Hakika tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha nyingi ambazo zimejenga miundombinu mbalimbali ikiwewemo kuboresha hospitali yetu ya wilaya, zahanati na vituo vya afya," ameshukuru na kuongeza kuwa:
"Tumeboresha Miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa shule mbili mpya za sekondari, ujenzi wa nyumba za maafisa ugani ili waweze kusimamia fani Yao kikamilifu kwenye sekta ya kilimo ndani ya kata zetu. Na Majengo yote yamekamilika na kuanza kutoa huduma, Hongerenii sana."
Pia, amesema Halmashauri imefanikiwa kutoa mikopo itokonayo na asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi hicho, kwa zaidi ya Tsh. 808.557 milioni kwa vikundi 65.
Akizungumzia Mpango wa kunusuru Kaya Masikini (TASAF), Bi. Selwa amebainisha walengwa 10,557 kutoka katika vijiji 119 na maeneo matano ya Mamlaka ya Mji Mdogo wamenufaika.
Amsema Halmashauri hiyo ilipokea Tsh. 14.771 bilioni zilitolewa kwa walengwa hao ambao waliibua miradi 80 ya kutoa ajira za muda.
"Wametekeleza miradi 59 ya barabara, visima sita, mabwawa, kivuko na mradi wa miti kwa asilimia 100," amedokeza.
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa idara na vitengo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, John Tesha amemuahidi Mkurugenzi huyo kuongeza ari na kasi ya kufanya kazi ili Halmashauri hiyo iendelee kujivunia utendaji wao wa kazi na kuweza kutoa matokeo chanya zaidi katika mwaka wa Fedha 2025/2026.
=================
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa