MKUU wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Mhe. Sauda Mtondoo amewaasa askari wa Jeshi la Akiba ambao wamehitimu mafunzo yao kuendelea kuwa waadilifu na wazalendo kwa Taifa lao.
Mhe. DC. Sauda ametoa wito huo leo Agost 28, 2025 wakati akifunga mafunzo hayo yaliyodumu kwa miezi mine katika kijiji cha Mwanzugi wilayani hapa.
Amewataka kuyatumia mafunzo waliyopata kuendelea kujilinda ikiwemo kulinda wananchi dhidi ya wahalifu na maadui kwa sababu kufanya hivyo jamii itaendelea kuwaamini.
Aidha, amewahimiza kutumia mafunzo ya ujasiriamali waliyoyapata kwa lengo la kuendelea kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Mhe. DC. amewakumbusha wananchi kuwa mchakato wa uchaguzi kwa hatua anuai unaendelea na kampeni zinaanza leo, hivyo wajiandae ifikapo Oktoba 29 mwaka huu wakapige kura kuchagua viongozi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mshauri wa Jeshi la Akiba wa wilaya hiyo, Meja Ayadi Amiri amesema askari waliohitimu ni 102 ambapo wanaume ni 84 na wanawake ni 18.
Ameeleza wahitimu hao wamejifunza mafunzo mbalimbali kwa nadharia na vitendo ikiwemo nidhamu, kwata, usalama wa raia, mbinu za kivita, ujanja wa porini, silaha ndogondogo na jinsi ya kupambana na rushwa.
Ameongeza mfunzo mengine ni pamoja na utimamu wa mwili, jinsi ya kujikinga na adui kwa kutumia singe, namna ya kumtambua adui kabla hajawatambua, shabaha, kareti, zimamoto na uokoaji, uhamiaji na sheria za usalama barabarani.
Aidha, Meja Amiri amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Selwa Abdalla Hamid kwa kufanikisha mafunzo hayo mwanzo hadi mwisho.
Kwa upande wa MG. Charles Taungiru amesema mafunzo hayo yamewajengea uzalendo, uadilifu, uaminifu, uvumilivu, ukakamavu na kuwawezesha kufahamu nia na moyo wa kulinda Taifa lao.
================
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa