MKUU wa Wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora, Sauda Mtondoo amewataka wanawake kufahamu pamoja na juhudi za kuendelea kupambania usawa, haki na uwezeshaji wanalo jukumu la msingi la kulea, kutunza na kulinda familia.
Aidha, wanawake wanayo kazi ya kufanya kwa lengo la kuimarisha haki sawa na wanaume katika nyanja mbalimbali za maisha.
DC Sauda ameyasema hayo jana katika Kongamano la Wanawake lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
Aliweka wazi kuwa katika suala la kutoa maamuzi, kumiliki ardhi na mirathi katika zile jamii ambazo zinaona Wanawake hawana haki ya kutoa maamuzi, kumiliki ardhi na mirathi.
‘’Tuendelee kutafakari kuimarisha haki na usawa katika nyanja ya uongozi na kutoa maamuzi hasa katika kipindi hichi ambacho Tanzania inapigiwa mfano kwa sababu inaongozwa na Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ’’ alisema.
Aidha, alieleza kuwa Wanawake wanapambana katika kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla huku akiwaasa kutosahau kulea na kutunza familia zao.
Aliongeza kuwa Mwananke akisimama imara basi familia itasimama vizuri lakini akitetereka na familia itayumba yumba, hivyo wanatafuta na kupambana kwa lengo la familia, ni vema wajue mwenendo wa watoto na waume wao.
‘’ Hivi sasa kunachangamoto kubwa katika malezi na makuzi ya watoto wetu kwa kuingia kwenye makundi mabaya, wanawake ndio nguzo za familia, hivyo tusimame imara kuhakikisha malezi na makuzi ya watoto wetu yako vizuri,’’ alisema.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Selwa Abdalla Hamid aliwakumbusha waandaaji wa Kongamano hilo kuhakikisha Kongamano lijalo Wanaume nao wanakuwepo kwa lengo la kuona nguvu ya Wanawake katika Halmashauri hiyo.
Alisema wanapeleka shukrani zao kwa Rias Dk. Samia kwa sababu amewachagua wao akiwaamini wanaweza kuongoza Wilaya ya Igunga kwa ushirikiano walionao.
‘’ Tunae Rais wetu ambae ni Mwanamke hivyo tunaweza kufanya chochote na popote ikiwemo kuwa Makamu wa Rais Mwanamke au Waziri Mkuu,’’ alisema na kuongeza kuwa:
‘’ Tunaweza kuleta mabadiliko, hivyo tuendelee kufanya kazi kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya kwa sababu tunauwezo mkubwa, tuendelee kujiamini na kuonesha umuhimu wetu.’’
Kongamano la Wanawake limefanyi ikiwa ni maandilizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika kimkoa Nzega Mji ifikapo Machi 08, 2025.
=== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa