MKUU wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Mhe. Sauda Mtondoo amepiga marufuku kwa AMCOS yoyote kupokea Pamba yenye maji, mchanga au mawe, hivyo itakayobainika kukiuka itachukuliwa hatua kwa sababu watakuwepo wataalamu watakaokua wanapima unyevunyevu ikiwemo mawe na mchanga.
Mhe. DC. Sauda ametoa kauli hiyo Jumanne Mei 13, 2025 wakati akiongea na baadhi ya wakulima, Viongozi wa AMCOS, Kampuni na Bodi ya Pamba katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
Aidha, amesema ni marufuku kwa viongozi wa AMCOS kwenda kupima Pamba ya mkulima nje ya kituo cha kununulia Pamba huku akisisitiza marufu kumlipa mkulima kabla ya kuleta Pamba kwa makubaliano kwamba atakapovuna ataleta Pamba.
‘’Avune Pamba yeke iletwe kituoni ipimwe na kukaguliwa ndio alipwe fedha zake kwa sababu ukishamlipa fedha kabla maana yake hata akileta pamba chafu utalazima kuipoeka kwa kuwa fedha yako alikwishachukua na hauwezi kuikataa,’’ ameeleza.
Amesema Mkulima atatakiwa kulipwa fedha taslimu kulingana na pamba aliyouza na kupewa risiti kwa sababu serikali imefanya mapinduzi kwa kuleta mizani ya kisasa inayohesabu kila kitu.
Akizungumzia kuhusu madaraja, ameweka wazi kutakuwa na madaraja mawili ambapo Pamba bora na Pamba Fifi huku bei elekezi ikiwa ni sh. 1150 kwa kilogramu moja ya Pamba Bora (daraja la kwanza) na sh. 575 kwa Pamba fifi, hivyo wakulima wanatakiwa kuzitenganisha Pamba zao kimadaraja kabla ya kufika kituoni.
Amedokeza kuwa Pamba ndio uchumi wa wilaya hiyo, hivyo nilazima wasimame imara na usimamizi uwe wa watu wote kwa lengo la kuendelea kuwaletea uchumi kwa Halmaashauri na wananchi wake.
Akizungumza katika kikao hicho, Mrajisi Msaidizi mkoani hapa, Evance Msafiri amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika ya mkoa huo kwenye msimu huu itachukuwa hatua kwa viongozi watakaobainika wameweka mchanga au maji na hivyo watakuwa wamekosa sifa yakuwa viongozi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Luca Bugota amewaomba viongozi wote kuilinda heshima waliopewa ya kuwa na Kitalu cha Mbegu huku akiwata kujiepusha na tamaa ambayo inaweza kuwapotezea heshima hivyo badala yake wadumishe uzalendo.
‘’Epukeni rushwa na tamaa ni adui wa hakiki, hivyo tubadilike na wale waliokuwa wakitegemea kupata rushwa kwenye pamba chafu sasa basi,’’amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri hiyo, Bi. Selwa Hamid amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais Dk. Samia Sukuhu Hassan kwa mema mengi aliyowafanyia katika wilaya hiyo ikiwemo kuletewa trekta, pembejeo na kiwanda cha kuchakata mbegu kwa lengo la kuongeza tija kwenye zao la Pamba, hivyo ni wajibu wao kutodhohofisha thamani ya zao hilo.
‘’Tuweke dhamira ya kweli msimu huu, ukiletewa pamba chafu mrudishe aliyekuletea na kumwambia kuwa Pamba hiyo haitakubalika, hivyo ukimrudisha mkulima mmoja tu salamu zitafika kwa wakulima wote,’’ alisema.
==== //// ==== //// ===
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa