MKUU wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Matiko Chacha ameendelea kuunga mkono michezo mbalimbali ikiwemo timu ya Igunga United ambayo iko mbioni kushiriki mashindano ya Mabingwa wa Mikoa jijini Arusha mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani hapa, Mhe. Sauda Salum Mtondoo alisema Mkuu huyo wa Mkoa baada ya kupata taarifa ya timu hiyo kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo alifurahi na kueleza kuwa anatambua mchango wa timu hiyo.
Aidha, Mhe. DC. Sauda aliwataka wachezaji wa timu hiyo kutambua wamebeba dhamana sio tu ya wilaya hiyo lakini ya mkoa huku akiwasisitiza kufahamu michezo ni ajira na nifuraha hivyo watakapokuwa uwanjani wambuke maneno haya kwa lengo la kuwatia ari ya kupata ushindi dhidi ya timu watakazokabiliana nazo.
‘’Ndugu Wachezaji, Mkuu wa Mkoa, Mhe. Paul Matiko Chacha amtoa sh. 1.5 milioni namimi ninawaongeza sh. 300,000 katika safari yenu hii, tambueni sisi viongozi wenu tuko nyuma yenu kwa lengo la kuhakikisha ushindi unapatikana,’’ alisema.
Pia, aliongeza wao wanathamini mchango wa timu hiyo katika michezo, hivyo wamebeba dhamana ya wilaya na mkoa wakafanye bidii kwenye michezo yao yote kwa lengo la kuhakikisha wanapata ushindi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Timu hiyo, Benard Daniel alieleza timu hiyo inauwakilisha Mkoa huo kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Mkoa huku ikiwa ni miongoni mwa timu nane bora.
Alisema wanakwenda jijini Arusha ambapo Aprili 23, 2025 wataanza mashindano hayo huku akitoa rai kwa wachezaji kuendelea kuupambania mkoa huo.
‘’Igunga United inatoka Igunga lakini kwa sasa inauwakilisha mkoa, hivyo wachezaji mnawajibu wa kuupambania mkoa kwa lengo la kuhakikisha timu inapanda daraja kutoka ligi dara la tatu kwenda daraja la kwanza,’’ alisema.
Aliweka wazi kuwa ni mashindano magumu lakini wanajiamini na wamejiandaa kupambana kulinda heshima ya viongozi wa mkoa na wilaya ambao wako bega kwa bega na timu hiyo.
Naye mchezaji wa timu hiyo, Deo Kaji alisema wamejiandaa vema kwa mashindano hayo wakiamini wanakwenda kuipandisha timu huku akiwaomba Mashabiki kuendelea kuwaunga mkono.
==== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa