Mkuu wa Wilaya ya Igunga Mhe. Sauda Mtondoo na wadau wengine wa Kilimo wamekutana kwenye kikao na kujadili mambo mbalimbali kubwa zaidi ikiwa ni kutangaza kitalu cha uzalishaji mbegu za Pamba katika gazeti la serikali na Wadau wamekubali kwa Kauli moja kwamba Igunga itangazwe rasmi kwenye gazeti la serikali kuwa kitalu cha uzalishaji mbegu za pamba.
Katika hotuba yake Mgeni rasmi Mh.Sauda Mtondoo amewaomba viongozi wa upande wa chama na serikali kuwa na uelewa wa pamoja hasa viongozi ngazi ya kata wote upande wa chama na serikali kwa kuhakikisha kwamba kila mkulima wa zao la pamba anazingatia kanuni bora za kilimo cha pamba.
"Sisi viongozi wa serikali tushirikiane na viongozi wa Chama ili tuwe na uelewa wa pamoja maana sisi tukiwa na uelewa huo na wenzetu wa chama wasipokua na uelewa hatutafanikiwa", amesema Mhe. Mtondoo.
Ameongezea kuwa serikali inavyoendelea kuboresha zao hili na uzalishaji nao unazidi kukua na kwa mwaka huu uzalishaji umefikia Tani takribani 26,000 ambayo inaipatia mapato Halmashauri karibu bilioni moja.
Kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga, kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali, wakulima na wadau wa kilimo sambamba na wadau kutoka Bodi ya Pamba Tanzania wakiongozwa na Mkurugenzi wake, James Shimbe.
Pamoja na mengi yaliyojadiliwa, upatikanaji na uzalishaji wa mbegu katika kitalu cha pamba kilichopo Wilayani hapa ni jambo lililotiliwa mkazo huku ujumbe kutoka Bodi ya Pamba ukiahidi kutoa ushirikiano kikamilifu kuhakikisha zao hilo linazalishwa kisasa na kwa ubora.
Aidha kikao hicho kimeweka mpango mkakati wa kuwatafutia usafiri baadhi ya watendaji, ili kuwarahisishia namna ya kuwafikia kwa urahisi wakulima sambamba na kuendeleza kuwaelimisha, kusimamia na kukuza uzalishaji wa zao la pamba.
Vilevile,imeshauriwa si vyema zao la pamba kuchanganywa na mazao mengine kwani hupunguza ubora wa pamba.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa