Mkuu wa Wilaya ya Igunga Mheshimiwa John Gabriel Mwaipopo juzi Januari 7, alizindua zoezi la upandaji miti kwa mwaka 2020 kwa kupanda mti katika eneo la wazi lililopo jirani na Hotel ya Dimax mjini Igunga katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira katika uzinduzi huo miti mia tatu (300) ilipandwa katika maeneo ya mji wa Igunga
Mheshimiwa Mkuu huyo wa Wilaya alizindua zoezi hilo akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vitangoji, Wakuu wa Idara na Vitengo , Wataalamu na Wananchi waliojitokeza kwa wingi ikiwa ni ishara ya ukubali na uendelezaji wa utunzaji na upandaji wa miti katika Wilaya ya Igunga
Akihutubia wananchi na wadau wote waliohudhulia uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya huyo alisema ”upandaji wa miti hiyo unahusu wananchi na kila kaya kupanda miti 5, kutunza kwa kumwagilizia maji miti hiyo na kuhakikisha miti hiyo inatuzwa na kila mtu kwa kuzingatia sheria za mazingira”
Aliendelea kusema miti inayopandwa itagawiwa bure kwa kila kaya ambapo jumla ya miti elfu tano (5000) imenunuliwa kwa gharama ya Tsh 2,112,500/= ikiwa ni pamoja na usafiri ambapo kufikia Januari 20, jumla ya miti 5000 inatarajiwa kupandwa katika Wilaya ya Igunga
“Nasisitiza ni lazima miti hiyo itunzwe na mda si mrefu maji yatakuwepo yakutosha katika wilaya yetu ya Igunga kutoka ziwa Victoria hivyo ni fursa kwetu sote sisi kama wakazi wa wilaya hii kutumia maji hayo kwa ajili ya utunzajiji miti hii na tutahakikisha kila mtu anakuwa mlinzi wa mwenzake katika utunzaji wa miti hii kama mfano bora ambao na Mkuu wa Mkoa wetu wa Tabora amekuwa akiuonyesha” alisema Mhe.Mkuu wa Wilaya
Aidha Mhe. Mkuu wa Wilaya aliendelea kuwataka wakazi wa Wilaya hiyo kuzingatia sheria za ufugaji wa mifugo mjini, ikiwa ni ufugaji wa kujenga mabanda na wala sio mifugo kuzagaa ovyo na kuharibu miti itakayopandwa na kusema sheria itachukua mkondo kwa wafugaji watakaokiuka kwa mifugo yao kutembea na kulanda landa ovyo mitaani
Alihitimisha kwa kusema halmashauri itasimamia kwa kuhakikisha maeneo mhimu ya taasisi za serikali na zisizo za serikali kuzishauri kwa kupanda miti ikiwa ni sera ya Taifa na Mkoa kwa ujumla “Shule, Makanisa na Miisikiti, pembezoni mwa barabara zetu hayo nayo ni maeneo mhimu ya upandaji miti tutawashauri kupitia wataalamu wetu ili kuhakikisha mji wetu unakuwa wa kijani”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Wakili msomi Bwana Revocatus L. K. Kuuli alisema katika zoezi hilo la upandaji miti litaleta tija kwa halmashauri kwa mji kupendeza na kuendeleza ikolojia kwa viumbe hai wote huku akisisitiza halmashauri kwa kushirikiana na wataalamu wake watalinda miti hiyo kwa kuendelea kutoa elimu na kusimamia sheria za mazingira
Katibu Tawala Wilaya ya Igunga ”aliwataka wakazi wote wa Wilaya Igunga kuhakikisha kila mmoja anakuwa na choo bora na msako utafanyika kubaini wananchi wasiokuwa na vyoo , wananchi kufyeka majani yanayozunguka makazi yao ili kufikia sera ya Zero malaria katika wilaya na vitongoji vyake” alisema Katibu Tawala Bwana.Godlove Kavishe
Akifafanua sheria na adhabu ya kushindwa kutunza mazingaira na miti Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Ndugu. Fredrick Mnahela alisema kwa yeyote anayeshindwa kutunza mazingira ipo sheria ya mwaka 2004 na.20 kifungu na.181 kitakachomshitaki ambapo mtuhumiwa anaweza kufungwa kifungo cha miezi sita gerezani, au faini ya kiasi cha shilingi elfu hamsini (50,000/=) hadi million hamsini (50,000,000/=)
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwayunge Ndugu. Milambo Gervasi amewapongeza viongozi hao wa serikali na kuipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuja na sera ya upandaji wa miti huku akisisisitiza miti hiyo italindwa na wananchi wote kwa kushirikiana na uongozi wa serikali za mitaa.
Mkoa wa Tabora umekuwa ukisisitiza swala la upandaji wa miti katika maeneo yake mbalimbali ya Taasisi na kando kando ya barabara zake na Mkuu wa Mkoa huo Ndugu. Aggrey Mwanry amekuwa msitari wa mbele kuhakikisha mazingira ya Mkoa huo yanakuwa ya kijani na zoezi hili kitaifa lilizinduliwa na Makamu wa Raisi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Desemba 25, 2017 akiwa Mkoani Dodoma na kutaka kila Mkoa kupanda miti kuanzia million moja na laki tano kwa kila Mwaka na kuwa zoezi la kudumu.
Picha na video zaidi ingia katika maktaba ya http://igungadc.go.tz/sinlge-gallery/uzinduzi-upandaji-miti-igunga
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa