Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Gabriel John Mwaipopo, amesema Mwenge wa uhuru 2018 Wilayani Igunga utatembelea miradi ipatayo mitano (5) kutoka Sekta za Elimu, Miundombinu ya barabara na Sekta Binafsi yenye thamani ya Tsh. 1,414,987,099/= alipokuwa akipokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mheshimiwa Godfrey Ngupula, katika Viwanja vya Ziba hivi karibuni.
“ Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 unatarajiwa kukimbizwa kilometa 138.4, katika Wilaya ya Igunga na utazindua Miradi mitano (5) yenye thamani ya shilingi bilioni moja milioni mia nne kumi na nne laki tisa themanini na saba elfu na tisini na tisa tu. Tsh.1, 414,987,099/=. Aidha mchanganuo wa uchangiaji wa fedha za miradi hii ni kama ifuatavyo: mchango wa Serikali Kuu ni Tsh. 512,068,099/= mchango wa Nguvu za Wananchi kupitia sekta binafsi ni Tsh. 902,919,000 /=” alisema Mhe, Gabriel J. Mwaipopo.
Aliendelea kusema Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mwenge wa Uhuru wilayani Igunga utakimbizwa kwenye Tarafa mbili za Manonga na Igunga na katika Kata saba za Ziba, Ibologero, Nyandekwa, Nanga, Igunga, Ugaka na Nkinga.
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2018 ambao unaojikita katika kuwahamasisha Watanzania kuwekeza katika elimu chini ya Kauli Mbiu isemayo: “Elimu ni Ufunguo wa Maisha; Wekeza Sasa kwa Maendeleo ya Taifa letu”, Wilaya yetu ya Igunga inaunga mkono kwa vitendo dhamira na juhudi hizi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha elimu katika ngazi zote Nchini kuanzia elimu ya awali hadi Chuo Kikuu.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa