MWENYEKITI Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Mhe. Shabani Hemed ameahidi kuiongoza Halmashauri hiyo kwa kasi itakayoiwezesha kukua katika nyanja ya uchumi, afya na huduma nyingine za jamii.
Mhe. Shaban ameyasema hayo Al hamisi Disemba 04, 2025 wakati wa Mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
"Ni wajibu wetu kushirikiana na wataalamu kuhakikisha tunatatua kila aina ya changamoto ikiwemo kusimamia miradi ya maendeleo," amesema
Aidha, amewahamasisha Madiwani kwenda kusimamia na kuongeza ufanisi wa kukusanya mapato, kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma huku akikemea wanaodaiwa kufuja, kuiba na kufanya ubadhirifu kuacha mara moja.
Pia, amewaomba kutoingia mikataba mibovu, na kuwa na mipango ya kuongeza kuzalisha mali katika kilimo, mifugo, viwanda, madini na biashara.
Katika hatua nyingine, Shabaan amewataka Madiwani hao kuwa mabalozi wa amani katika kata zao ikiwemo kuwaelimisha vijana, wazee na watoto wao kuwa amani ndio msingi wa maendeleo.
Awali akiwasilisha taarifa ya kumbukumbu ya maamuzi na utekelezaji wa shughuli za Halmashauri hiyo, Kaimu Mkurugenzi, John Tesha amesema katika mwaka wa fedha 2025 hadi 2926 Halmashauri imekusudia kutumia sh 57.3 bilioni ambapo hadi kufika Novemba 30, imekwishatumia sh. 18.8 bilioni sawa na asilimia 31.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Manonga wilayani hapa, Mhe. Abubakar Alli amewataka Madiwani hao kutofanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa kasi na kujituma kwa sababu wananchi wananchi wanataka matokeo ya suluhisho la matatizo yao na sio sababu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Igunga, Mhe. Charles Kabeho ameeleza kuwa ataendelea kutoa ushirikiano kwa lengo la kuhakikisha wanafanya kazi ambazo Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amezikusudia katika wilaya hiyo.
Akizungumza katika Baraza hilo, Diwani wa Kata ya Bukoko, Jidashema Mwandu amewapongeza viongozi wa Halmashauri kwa kukusanya mapato ambayo yamevuka malengo.
============

Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa