NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amemkabidhi Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Hamisi H. Hamisi Tuzo ya Usimamizi bora wa Rasilimaliwatu.
Mhe. Naibu Waziri amemkabidhi tuzo hiyo wakati wa Kikao cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika Hoteli ya Halmashauri ya jiji la Dodoma jijini humo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Watumishi wa wilaya hiyo, wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Selwa Hamid ambae amekua akishirikiana vema na Mkuu wa Idara hiyo, Hamisi H. Hamisi kutoa huduma bora kwa watumishi, Madiwani na wananchi kwa ujumla.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Michezo na Utamaduni wa Halmashauri hiyo, Fadhil Kayange amesema ameipokea tuzo hiyo kwa furaha kwa sababu wameipata kutokana na hekima, busara na nidhamu ya kazi iliyopo kwa viongozi wao.
‘’Hakika viongozi wetu ni wasikivu wa changamoto zote zinazodaiwa kuwapata watumishi, binafsi ni mnufaika wa huduma bora wanazozitoa viongozi wetu ikiwemo kubadilishiwa muundo wa utumishi kutoka Mwalimu na kuwa Afisa Michezo Msaidizi, hivyo ninawapongeza na wanastahili tuzo hii,’’ amesema.
Kwa upande wa Afisa Mifugo Msaidizi Mkuu wa Halmashauri hiyo, Mohamed Kiswamba aliweka wazi kuwa wameipokea tuzo hiyo kwa furaha kwa sababu wanastahili kwa namna ambavyo wanachapa kazi kwa ushirikiano na ushirikishwaji kati yao na viongozi wao.
‘’Ninatoa wito kwa watumishi wenzangu wakiwemo viongozi wote tuendelee kuchapa kazi kwa kushirikiana kwa lengo la kueendelea kuonekana mfano wa kuigwa katika uongozi bora ikiwemo kukusanya mapato na kutoa huduma bora kwa wananchi,’’ amesema Kiswamba.
Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Mwanzugi, Yohana Uhwelo ameeleza kuwa wameipokea tuzo hiyo kwa kishindo chenye uhalisia kwa sababu wamekuwa wakihudumiwa vizuri na Idara hiyo kutokana na ushirikano na uongozi bora, hivyo wanachapa kazi na wanaona ni haki yao.
Akiongea kwa njia ya Simu Mkuu wa Idara hiyo, Hamisi H. Hamisi amefafanua kuwa wamepata tuzo hiyo kwa sababu wamekuwa wakitekeleza vigezo vya Usimamizi wa Kanuni, Usimamizi mzuri wa Mifumo ya Kiutumishi, Usafi wa Mifumo, Utekelezaji wa Maagizo ya Viongozi na Usafishaji wa Taarifa za Watumishi.
Kufuatia tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Selwa Abdalla Hamid amesema ni jambo la kujivunia huku akiwapongeza watumishi wote na kuwataka kuendelea kuchapa kazi kwa weledi, maarifa, juhudi na busara kuwahudumia wananchi.
======/////=====/////=====/////=====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa