MWAKILISHI wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Jasper Tito amewaomba wachimbaji hao kupokea ujumbe wa tozo walioelezwa.
Tito ametoa ombi hilo Agosti 26, 2025 wakati akiongea na Wachimbaji wa kijiji cha Igurubi wilayani hapa.
"Niwaombe pokeeni tozo hizi na maoni yenu tumeyachukua, hivyo tutayafanyia kazi," ameeleza.
Akizungumza katika mkutano huo, Ofisa Maliasili na Mazingira, Emmanuel Mnanka amewahakikishia wachimbaji hao kuwa wataendelea kulifuatilia kwa viongozi wao, hivyo wanaweza kupata soko la kuchomea na kuuza dhahabu.
Aidha, akiongelea kuhusu tozo Mnanka amesema tozo hizo zikikusanywa zitaendelea kuboresha miundombinu mbalimbali itakayoendelea kuwanufaisha wananchi .
Kwa upande wa Mchimbaji, Emmanuel Banturaki amesema tozo mbalimbali zitokanazo na madini zinalipwa.
"Mwalo na Karasha ni vitendea kazi vyetu katika uchimbaji wa madini kwanini vitozwe kodi ?," amehoji.
Naye Jagadi Masunga amesema serikali kubuni vyanzo vya mapato sio vibaya, hivyo ameomba Wataalamu warudi waangalie upya vyanzo hivyo kwa sababu wachimbaji wanakata mitaji na kurudi kwao kwa sababu kuna hasara wanaipata.
Mayunga Kwilasa ameiomba serikali iendelee kukaa na wachimbaji kwa lengo la kuelewa changamoto zao watabaini changamoto wanazozipitia na kuwapunguzia huo mzigo wa kodi.
"Ni kweli nchi inaendeshwa kwa tozo na kodi, hivyo serikali iendelee kutuwezesha tukizalisha zaidi hakuna mtu atakaepinga kutoa kodi na tozo," ameshauri.
Naye Magese Balele amesema wanaomba wapate soko badala ya kwenda kuuza dhahabu Nzega wauze Igunga.
"Jengeni sehemu za kuchomea dhahabu Igunga kwa lengo la kuhakikisha fedha tunazozipata tunazitumia Igunga nasio Nzega," amesema.
====== //// ======
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa