WANANCHI wa Wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora wameunga mkono kivitendo kampeni ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi baada kujitokeza kwa wingi kununua mitungi ya gesi na kuahidi kuachana na matumizi ya nishati chafu.
Akizungumza jana baada ya kununua nishati hiyo, Prisca Onesmo alisema wanaachana na matumizi ya kuni kwa sababu zimekua zinawaletea athari kwenye macho wanapokua wakipuliza moto wakati wa kupika.
Aidha, aliwashauri wanawake wanaotumia kuni waache kwa sababu serikali ya Rais Dk. Samia imetoa ruzuku kwenye nishati hiyo, hivyo mtu akiwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na sh. 20, 000 anapata mtungi wa gesi.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Nguvumoja wilayani hapa, Afred Nkuba alieleza kuwa Kampeni ambayo ameianzisha Rais Dk. Samia inawasaidia kwa sababu awali walikua wananua tela moja la kuni kwa sh. 50,000 huku gunia la mkaa wakinunua kwa sh. 30,000, hivyo nishati ya gesi kuuzwa bei hiyo inawasaidia kuachana na matumizi ya nishati chafu ambayo licha ya kuwadhuru ni ghali kuipata.
‘’Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia kwa kampeni hii kwa sababu inawapunguzia wananchi kukata miti katika mapori yaliopo katika wilaya yetu,’’ alisema.
Naye Msimamizi wa Kampuni ya Gesi ya ORYX kanda ya Magharibi, Gibson Rodgers aliweka wazi kuwa wameisha uza majiko 13, 820 katika mkoa huo huku kwa upande wa wilaya ya Igunga wakiuza majiko 3255.
Pia, alieleza thamani halisi ya majiko hayo ni sh. 50, 000 lakini wameiuzia serikali kwa sh 40,000 ambapo Rais Dk. Samia emeweka ruzuku ya sh. 20,000 hivyo wanawauzia wananchi nishati hiyo kwa sh. 20, 000 tu.
Kufuatia fursa hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Lucas Bugota aliwaomba wananchi waendelee kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia na kumpa tena miaka mitano kwa sababu wanakinama wanajua kulea.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Halmashauri hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sauda Mtondoo alisema Rais Dk. Samia anamaono makubwa ya namna ya kuwakomboa wananchi kuacha kutumia nishati chafu badala yake wajikite katika matumizi ya nishati safi.
Alieleza kuwa Dk. Samia amekua mtu wa mbele (Champion) na kushika nafasi ya pili barani Afrika, hivyo wanakila sababu ya kuhakikisha wanamfanya awe namba moja Afrika.
Aliwahimiza wananchi kuelekeza nguvu zao katika matumizi ya nishati safi kwa sababu wanaamini itakuwa ni suluhisho la kutunza mazingira na kuwaokoa akinamama na maradhi yanayotokana na matumizi ya nishati chafu.
==== //// ==== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa