UMOJA wa Wanawake wa Wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora wamefanya zaira ya kuwatembelea na kuwashika mkono wagonjwa mbalimbali waliopo katika Hospitali ya Wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Wanawake.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Afisa Tarafa wa Kata ya Igunga, Advella Kakuru aliwashukuru Wanawake hao kwa namna ambavyo wamejitoa kwa lengo la kuhakikisha wenzao waliokua katika halimbalimbali wanakuwa na furaha mfano wa waliyonayo wao.
‘’Leo tukiwa tunaelekea kuadhimisha siku ya mwanamke duniani umoja wetu umeona uwashike mkono kwa sababu sisi sote ni akinamama, hivyo tunaelewa ilivyo kazi kulea na kuuguza,’’ alisema na Kuongeza kuwa:
‘’Chochote ambacho mmechanga na mmetoa kwa wenzetu hawa tunamuomba Mwenyezi Mungu awalipe badala, hivyo tuendelee na umoja huu kwa lengo la kuhakikisha mwakani tunayafikia makundi mengine wakiwemo watoto yatima na wafungwa.’’
Aidha, aliwaomba wagonjwa kuendelea kuwa na faraja kwa sababu wanawake wote waliowatembelea wanawatia moyo na wanaamini Mwenyezi Mungu atawafanyia wepesi na watapona maradhi yanayowasibu.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Grace Nyamwanji alisema wameungana na Wanawake walipo Wodini ambao wanauguza kuwashika mkono kwa baadhi ya mahitaji kwa lengo la kuwaweka karibu wasijisikie upweke.
‘’Tunaomba mfahamu sisi tuko pamoja na nyinyi kwa sababu sisi sote ni walezi na tuliishawahi kuuguza, hivyo jisikieni faraja tuko pamoja,’’ alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Afisa Afya, John Masesa aliwapongeza Wanawake hao kwa sababu matendo ya huruma waliyoyafanya ni makubwa na niibada.
Aidha, alisema kazi ya Mama katika jamii ni kubwa kwa sababu kama si akinamama wasingekuwepo, hivyo waendelee kuwaombea akinababa kwa lengo la kuhakikisha Wanakaa sawa.
‘’Ninashukuru sana na kuwaomba muendelee kutulea na kututunza kwa sababu ni moja ya wajibu wenu na tuombe jamii iendelee kuwa na afya njema itekeleze majukumu yake,’’ alisema.
Kwa Upande wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Scholastica Ikandilo alieleza kuwa wanajitahidi katika kutoa huduma bora, hivyo kuna mabadiliko makubwa kwa sababu Wauguzi walionao wanatekeleza maadili ya kazi zao.
‘’Nitoe wito kwa jamii wanapokua na ushauri wasisite kutueleza na sisi tutaufanyia kazi kwa sababu sisi tulipata elimu hizi kwa lengo la kuhudumia jamii na sio kukaa na elimu zetu nyumbani,’’ alitoa wito.
Naye mmoja wa Wazazi, Hadija Shabani aliwashukuru Wanawake hao kwa kuwajali na kuwathamni huku akiwaomba wasisite kuendelea na moyo huo.
‘’Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaongoza kuja kututembelea wanawake wenzenu ninamuomba Mungu awabariki na kuwaongezea kwa kile mlichotoa,’’ alishukuru.
Umoja wa wanawake huo, umemtembelea Hadija Shabani mama wa Mapacha walikua wameungana na kutenganishwa ambao kwa sasa wanaishi Nkokoto Igunga na kuwatembelea wagonjwa Wodi ya Watoto chini ya miaka mitano, Wodi ya watoto wagonjwa na waliolazwa na uzito pungufu (NICU) , Wodi ya Wazazi wanaotarajia kujifungua , waliojifungua na ICU.
==== //// ==== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa