KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Mhe. Dk. Khamis Mkanachi amesema Wanawake ni kundi kubwa katika jamii linaloongoza kwa wingi sio tu Tanzania mpaka duniani.
Dk. Mkanachi ameyasema hayo leo Jumamosi Machi 8, 2025 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliofanyika Kimkoa katika uwanja wa Samora Nzega Mji.
Alisema mazingira nchini ni rafiki, hivyo Wanawake wenyewe waendelee kuangalia namna wanawezaje kupata haki na usawa wanaoutaka ikiwemo kukabiliana na mambo ya kiuchumi.
"" Ndugu zangu ninamnukuu Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa Wanawake sio dhaifu, wanawake ni Mahiri, shupavu na wananguvu ," alinukuu.
Aidha katika kuwawezesha kiuchumi, alisema mkoa huo umewawezesha Wanawake hao mikopo ya asilimia 10 kutoka mwezi Januari mwaka 2024 hadi mwezi Machi 2025 sh. Bilioni 3.9.
Alifafanua kuwa Vikundi vya Wanawake 226 vilipata takriban sh. bilioni 1.9, vijana vikundi 127 walipata sh. bilioni 1.7 huku walemavu vikundi 32 wakipata sh. milioni 265.5.
Katika hatua nyingine, Dk. Mkanachi aliweka wazi kuwa Mwanamke ndio mwalimu wakwanza wa kiumbe yoyote anayekuja duniani.
"Mwanamke ni kama mwalimu, anasimama kama afisa mipango nyumbani, mchumi mwenye kujua bajeti ndogo na kubwa ya uwekezaji, mratibu wa mambo yote ya kifamilia na ni afisa uhusiano anayejenga na kuwaunganisha kati ya ndugu na watu wengine, familia na ukoo ikiwemo lugha nzuri ambayo ni tiba ndani ya familia," alisema.
Hata hivyo, aliwakumbusha wazazi pamoja na kutafuta fedha wasisahau malezi ikiwemo kuwasikiliza watoto na kuwalinda dhidi ya mmomonyoko wa maadili.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi, aliwashajiisha wajitokeze kugombea na kupiga kura kwa wingi wakiamini kwa wingi wao watapata ushindi wa kishindo.
"Niwaombe wanawake wote tumuahidi Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ushindi wa kishindo kwa sababu kura zake sio za mashaka kwa idadi ya wingi wa wanawake," aliahidi.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8 Mwezi Machi ya kila mwaka.
==== //// ==== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa