KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Joseph Mafuru amewataka Watumishi wa Afya kuendelea na zoezi la kuchanja kupitia huduma Mkoba kwa lengo la kuhakikisha wanafikia malengo ambayo waliyojipangia.
Mafuru ametoa wito huo wakati wa Kikao cha tathmini ya chanjo kwa watoa huduma za Chanjo wa wilaya hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Rufaa Nkinga mjini hapa.
Aidha, aliwahimiza kuendelea kuchukua taarifa za majukumu yao ikiwemo zoezi la chanjo na kudhihifadhi kwa lengo la kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo kutoa ripoti iliyochini ya hitajio ikiwa watakuwa na utaratibu wakutohifadhi taarifa zao.
‘’Ni lazima tuwe na matumizi sahihi ya fedha za chanjo ambazo zinamiongozo yake nakutotumia kwa matumizi mengine ikiwemo kununua umeme jambo ambalo linaweza kusababisha hoja,’’ alisema.
Katika hatua nyingine, Mafuru aliwasisitiza kuhakikisha wanapeleka fedha benki kwa kuzingatia miongozo iliyopo kwa lengo la kuepuka kutumia fedha mbichi.
Mkuu wa Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Lucia Kafumu aliwataka Watumishi hao kuwashirikisha Watendaji Wakata (WEO), Watendaji wa Vijiji (VEO), Waganga wa Tiba Asili ikiwemo kuhudhuria vikao vya Wazazi kwa lengo la kufikisha taarifa mbalimbali zikiwemo za chanjo.
Akizungumza katika kikao hicho Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Halmashauri hiyo (DIA), David Bakilile aliwaeleza kuwa ukaguzi wa kipindi cha nyuma uko tofauti na wa hivi sasa kwa sababu ni shirikishi na wanatoa elimu kisha ndio wanakuja kuwakagua.
Kwa upande wa Mwekahazina wa Halmashauri, hiyo Mpakani Kalinga aliwahimiza kuendelea kufuata taratibu za matumizi sahihi ya fedha ikiwemo utoaji wa taarifa.
‘’Sisi Wahasibu tunawategemea kuhakiksha kanuni na taratibu za fedha zinafuatwa katika vituo na Zahanati ambazo mnazisimamia, hivyo tutaendelea kuwapa mafunzo ya marara kwa mara kwa lengo la kuwanoa muwe imara kwenye usimamizi wa fedha,’’ alisema.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Wakuu wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya wa wilaya hiyo, Ramadhan Murad alishukuru uwepo wa viongozi wao ambao unazidi kuwahamasisha kuendelea kufanya vema ikiwemo Huduma Mkoba.
==== //// ==== //// ==== //// =====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa