MAENDELEO ya Sayansi na Teknolojia yanayoendelea kutekelezwa nchini hususan katika kutumia mifumo mbalimbali kutekeleza majukumu yamewaibua Watendaji wa Kata na Vijiji wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora kuiomba Serikali kuwatazama watumishi hao.
Wakizungumza katika kikao Kazi jana, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo chenye lengo la kijifundisha mfumo wa FFARS, Watumishi hao wameomba kupatiwa nyenzo za kisasa ikiwemo vishikwambi kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko hayo.
Mtendaji wa Kijiji cha Mwaomba kata ya Igurubi wa wilaya hiyo, Baraka Julias alisema wanaiomba serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI iwakumbeke Watendaji wa Kata na Vijiji kuwapatia vifaa vitakavyowawezesha kupata mifumo waliyofundishwa.
Kwa upande wa Mtendaji wa kijiji cha Mwakabuta, Revocatus Shamba aliishukuru Idara ya Fedha kwa kuendesha mafunzo hayo na kuomba Watendaji wa Vijiji na Kata wawezeshwe kupata Vishikwambi.
‘’Mafunzo haya yamenijengea uwezo, nimetambua dunia imehama kutoka analoji kuwa dijitali, hivyo ninaomba Watendaji wa Vijiji tuwezeshwe Vishikwambi,’’ aliomba.
Mtendaji wa Kata ya Ziba wilayani hapa, Daniel Jinge aliomba kuhusu mifumpo inayoongezeka ni vema wakaendelea kupewa mafunzo kwa lengo la kuendelea kuongeza ufanisi katika majukumu yao.
Kutokana na maombi hayo, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wilayani hapa, Mpakani Kalinga aliweka wazi namna ambavyo Utawala umejipanga kuitatua changamoto hiyo ya kutokua na Vishikwambi kwa kipindi hichi kwa kuanzisha chumba maalumu ambacho Watendaji watakitumia kufanya maandalizi ya malipo, kusainisha kisha kwenda benki.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wilaya hiyo, Hamisi Hamisi aliwataka Watendaji wanaodaiwa kuwa na tabia ya ulevi, uvivu na majibu mabaya kwa wananchi kuacha tabia hiyo.
‘’Serikali inawajali watumishi, hivyo kwa nini mshindwe kuwahudumia Wananchi vizuri, mliomba kazi kafanyeni kazi, hivyo sipo tayari kusikia migogoro ambayo ilitakiwa itatuliwe katika ngazi zenu inaletwa Halmashauri,’’ alisisitiiza.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Grace Nyamwanji aliwataka Watendaji hao kwenda kufanya usuluhishi wa fedha zilizoko benki kwa kulinganisha taarifa zilizopo katika vitabu vyao na kuziwasilisha kabla ya tarehe 7 mwezi huu.
‘’Ninawasisitiza ndugu viongozi mmepewa mafunzo haya mwende mkatekeleze hili kwa wakati,’’ alihimiza.
Mafunzo ya Mfumo wa FFARS kwa Watendaji wa Kata 35 na Vijiji 119 yalihusisha mada ya Mapokezi ya Fedha, Usuluhishi wa Kibenki, Kufanya Usuluhishi katika Mfumo na Maelezo kuhusu Mfumo wa Nest.
==== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa