WAFAWIDHI wilayani Igunga mkoani Tabora wamekutana katika kikao kazi Alhamisi Jaunuari 16, 2025 katika ukumbi wa St. Leo kujadili Bajeti, Matumizi ya Fedha, Bima ya Afya ya Taifa (NHIF), Taarifa ya Mapato robo ya kwanza na ya pili mwaka 2024 hadi 2025 ikiwemo maelekezo ya namna ya kupokea fedha kwenye mfumo na kufanya usuluhisho wa fedha zilizoko benki na matumizi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Selwa Abdalla Hamid ambae alikua mgeni rasmi katika kikao hicho alianza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kuijali Halmashauri hiyo kwa kuipatia fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo.
‘’Ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuwezesha kwenye rasilimaliwatu, kiuchumi, miundombinu na kupata fedha sh. milioni 100 za kuwakopesha Wajasiriamali wadogowadogo,’’ alishukuru.
Pia, aliwapongeza Waganga Wafawidhi na Watumishi wote wa Afya kwa namna wanavyotoa huduma za afya vizuri kwa wananchi, hivyo kuwahakikisha kwamba kadri wanavyoendelea kutimiza wajibu wao ndivyo utawala utakavyoendelea kuwajali.
Aliwahimiza kuhakikisha wanapeleka fedha zitokanazo na mapato kutoka kwenye vituo vyao benki na kuhakikisha zinasoma kwenye mfumo kisha waziombe kwa kufuata muongozo uliopo kwa lengo la kuendelea kufanya matumizi.
‘’Asiruhusiwe mtu yoyote kuchukua fedha ambayo haijaingizwa kwenye mfumo na kupelekwa benki,’’ aliagiza.
Pia, aliwakumbusha kuendelea kufanya usuluhisho wa kifedha kati ya zile zilizopo benki na matumizi kwa wakati kwa sababu tabia hii itawaondolea mzigo, hivyo wataweza kutekeleza shughuli zao kirahisi.
Aliwataka kuhakikisha wanaendelea kuwasimamia watumishi waliopo katika vituo vyao kwa lengo la kuendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa rasilimali watu.
‘’Mmepewa majukumu simamieni na ikitokea kuna mtumishi amekiuka taratibu au anawaharibia kazi mwambieni na msimuonee aibu kwa sababu msipo chukua hatua atawaharibia kazi,’’ alishauri.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Lucia Kafumu aliwakumbusha Wataalamu hao kuwa wamefanya kikao kazi hicho mwezi Januari kwa lengo la kupeana mwelekeo wa namna ya kuendelea kutoa huduma vema na waweze kutembea pamoja.
Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Halmashauri hiyo, Hamisi Hamisi aliwahimiza Watumishi hao kuendelea kuwa waaminifu, kuepuka rushwa, kuepuka unyanyasaji wa kijinsia, kuziishi kanuni za utumishi wa umma na kuwa na matumizi sahihi ya madaraka.
‘’Ndugu Watumishi wenzangu niwaombe tuendelee kujichunga na vitu vinavyoaibisha Utumishi wa Umma ikiwemo ulevi, kamari, kugombana na kubeti,’’ alionya.
Naye Afisa Tabibu wa Zahanati ya Mwanyagula, Ramadhan Murad aliahidi kuyafanyia kazi mambo yote yaliozungumzwa katika kikao hicho ikiwemo kuendelea kutoa huduma rafiki kwa wananchi.
‘’Tukuahidi Mkurugenzi wetu tutakusanya vizuri mapato, tutabenki na kufanya usuluhishi wa kifedha kati ya matumizi na fedha zilizopo benki kwa wakati,’’ aliahidi.
==== //// ==== //// ==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa