WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi imara ambae amedhamiria kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia katika maeneo yao.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo Jumatano Machi 12, 2025 kwa nyakati tofauti alipofanya ziara wilayani Igunga mkoa wa Tabora kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo
Akizungumza kuhusu mradi wa maji ambao aliuzindua, amesena mradi huo unagharimu sh. Milioni 840.8 na utawahudumia wananchi 5,402 wa kijiji cha Mwamayoka wilayani hapa.
Amewahakikishia wananchi hao, Serikali
inaendelea kusimamia kutoa huduma za maji safi na salama nchini kwa lengo la kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji inawafikia wananchi kwa asilimia 100.
“Ndugu zangu wananchi, mradi huu ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, hivyo kuweni na uhakika kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayewajali, anawapenda na anasikiliza changamoto zenu, endeleeni kutekeleza majukumu yenu ipasavyo kwa sababu tunaye kiongozi madhubiti” amesema.
Mbali na hayo, Majaliwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha sekta ya mifugo inakuwa endelevu na yenye tija.
Amesema kuwa Mhe. Dkt. Samia muda wote ameweka msisitizo katika kuiendeleza sekta hiyo kwa kuwa mifugo ni uchumi, ajira na ni biashara.
“Tunawahamasisha wafugaji, fugeni mifugo ni uchumi, mifugo ni maisha na mifugo ni pesa na wakulima limeni tupate mazao mengi ya chakula na biashara," amesema.
Aidha, ameziagiza Halmashauri zote nchini kuweka mikakati ya kuhakikisha wanakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuzisimamia fursa zilipo kwenye maeneo yao kwa lengo la kuwanufaisha wananchi.
Kwa upande wa elimu, ameitaka jamii kuweka nguvu za pamoja katika kumlinda mtoto wa kike kwa lengo la kuhakikisha waweze kutimiza ndoto zao.
Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati iliyopo katika sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha sekta hiyo iweze kuwanufaisha watanzania kwa kukuza ubora wa elimu nchini.
Waziri Mkuu mefanya ziara Igunga na kuweka jiwe la msingi Mradi wa Upanuzi wa Mtandao wa Majisafi ya Ziwa Victoria kutoka Makomero - Mgongoro, uliopo kijiji cha Mwamayoka, jiwe la msingi kwenye shule ya Sekondari ya Seif Gulamali, ametembelea mradi wa vibanda 80, kuweka jiwe la msingi upanuzi wa mradi wa maji Ziwa Viktoria awamu ya pili na kuongea na wananchi Simbo.
==== //// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa