Kwa ufadhili wa shirika la World Vision limezindua timu hiyo ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ambayo itakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa Haki za mtoto zinazingatiwa na kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria.
Uzinduzi huo ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga aliyewakirishwa na Katibu Tarafa Igunga ndugu Shadrack Pastory Kalekayo, iliyofanyika katika ukumbi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga tarehe 05 Juni, 2017 na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali ambao ni wadau wa watoto wakiwemo Wataalam wa Halmashauri (kutoka Idara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Elimu, Mipango), wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ( Mkuu wa gereza la Igunga, Mshauri wa Mgambo, Afisa Uhamiaji na Dawati la jinsia Polisi), mwakilishi wa NGOs, Wawakilishi wa madhehebu ya Dini na mwakilishi wa Walimu.
.Akizungumzia kuundwa kwa timu ya ulinzi na usalama wa mtoto, Shadrack kalekayo, alisema kutakuwa na faida kubwa baada ya kuanza kutekelezwa kwa mpango huo kwa ushirikiano wa Halmashauri na ufadhili wa Shirika la World Vision.
Aliongeza kuwa faida ya kuundwa kwa timu hii ni itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili wanaofanyiwa watoto katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani, migodini, mashamba ya kilimo cha umwagiliaji n.k, baadhi ya ukatili wanaokutana nao watoto ni pamoja na ukatili wa kihisia ambapo mtoto anakutana na matusi, kinyimwa chakula, kuto thaminiwa, ukatili wa kimwili inaambatana na vipigo,kukatwa viungo vya mwili, kuchomwa moto, kutumikishwa, ukatili wa kingono inahusisha kubakwa, kulawitiwa, na ndoa za utotoni.
Shadrack aliendelea kwa kusisitiza kwamba timu ikasaidie kuelezea Suala la ulinzi wa mtoto kuwa ni jukumu la jamii nzima, mlezi na mzazi mmoja mmoja kwa nafasi yake katika ngazi ya familia pamoja na serikali kwa ujumla. Ushirikiano katika malezi ya mtoto kati ya wazazi, walezi pamoja na jamii unahitajika kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha usalama wa mtoto. Sehemu nyingine ya muhimu ni ushirikiano na mahusiano ya karibu kati ya mwalimu na mzazi ili kuhakikisha miendendo ya mtoto darasani, mtaani hadi nyumbani.
Akahitimisha kwa kusema, Ieleweke kwamba mzazi, jamii na serikali tukishirikiana hatuwezi hata siku moja kuwaona watoto wakiwa mitaani wanazurura muda ambao wanatakiwa kuwa kwa wazazi wao au shuleni nasi tukabaki kimya. Tuhoji pale tunapowaona madukani wakinunua vilevi, sigara, n.k. Vinginevyo tutarajie ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, watoto wanaotumia madawa ya kulevya, watoto wanaojihusisha na biashara ya haramu ya ngono, n.k.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa