Idara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya wilaya ya Igunga, ilikuwa sehemu ya Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika. Iliundwa rasmi mwaka 2012/2013, kutokana na agizo la serikali la kutaka iwe Idara inayojitegemea ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi kwa sekta hii muhimu. Lengo kuu la Idara hii ni kusimamia na kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi, ili ziwe zenye tija, ufanisi na ushindani, zinazochangia kuboresha hali za wananchi wa wilaya ya Igunga ambao ufugaji na uvuvi ni sehemu ya shughuli zao za kila siku na zenye kuzingatia hifadhi ya mazingira. Malengo mahsusi ya Idara, ni pamoja na kuboresha koosafu za mifugo ya asili, kuboresha malisho ya asili na kudhibiti matumizi bora ya ardhi, kuzuia na kudhibiti magonjwa ya mifugo na kuboresha masoko ya mifugo na mazao yake. Majukumu ya idara ni pamoja na kuratibu, kusimamia, kufuatilia, kutekeleza Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Maagizo yanayohusu shughuli zote za maendeleo ya sekta za mifugo na uvuvi, kwa kushiriki na kushirikisha wadau wote wa maendeleo na hifadhi ya mazingira.
Idara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi inaundwa na sehemu mbili, yaani mifugo na uvuvi, zenye wataalam wa fani mbalimbali, zikiwemo, udaktari wa wanyama, sayansi ya uzalishaji wanyama, sayansi ya uzalishaji, utumiaji, hifadhi na uendelezaji wa nyanda za malisho, wataalam wa wanyama wadogo, kuku, masoko ya mifugo na mazao yake, tiba na afya ya mifugo, uhimilishaji, uanzishaji na uendeshaji wa mashamba darasa ya mifugo, usimamizi na ufuatiliaji wa program za ugani. Idara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ina jumla ya watumishi 34, ambapo watumishi 9 wapo makao makuu ya wilaya na wengine 25 wapo ngazi ya kata. Shughuli wanazofanya wataalam hawa ni pamoja na kutoa ushauri wa ufugaji bora wa mifugo na samaki, kuwezesha uundaji wa vikundi na vyama vya wafugaji, kuratibu, kusimamia na kufuatilia afya ya mifugo, kinga na matibabu ya mifugo, ukaguzi wa nyama na usafi wa machinjio, kukusanya maduhuli ya serikali, kuratibu, kusimamia na kufuatilia masoko ya mifugo na samaki, kukusanya takwimu za mifugo na mazao yake na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni, miongozo na maagizo yanayohusu maendeleo ya sekta za mifugo na uvuvi wilayani.
Majukumu ya Idara ya Mifugo na Uvuvi
Nb: Wataalam waliopo wilayani ni Dr. Emmanuel Masaki (BVM -VO I) – Afisa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (W);Mr. Andreas Kafuru (BSc. An. Sc. AHD, AHPC -SLO) – Afisa Mifugo (W); Mr. Steven Mdaki (MSc. Agr. Ext. Educ, BSc. Range Mngt, AHD.-LO I) SMS (Uendelezaji nyanda za malisho);Mr. Paul Mtani (Dip. Range Mngt.-PLFO I) – Afisa Masoko ya mifugo; Ms Martha Rwiza (Dip. Poultry Prod.-PLFO I) SMS (Uzalishaji kuku na wanyama wadogo wadogo);Mr. Mohamed Kiswamba (AHD-LFO I) SMS(Afya ya Mifugo na udhibiti magonjwa ya mifugo): Mr. David Sengo (AHD-PLFO I) Focal person (Ngozi): Mr. Ezra Lema (AHD-PLFO I) – Afisa Ugani (W): Mr. Lazari Mushi (Dip. Range Mngt.-PLFO I) Kaimu Afisa Uvuvi (W).
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa