BARAZA la Madiwani wilayani Igunga mkoani Tabora limempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa mgombea pekee kwa nafasi ya Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi 2025.
Pongezi hizo zimetolewa Jumatano Januari 29, 2025 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024 hadi 2025 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Lucas Bugota alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuwaletea katika wilaya hiyo viongozi waadilifu na kufanya mambo makubwa kwa sababu hakuna Diwani ambaye Kata yake haijaguswa na pesa za Mama Samia.
‘’Na sisi Baraza la Madiwa na Wataalamu wetu tunaunga mkono tamko la Mkutano Mkuu Maalumu wa Dodoma uliofanyika tarehe 18 na 19 mwezi huu kumteua Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee kwenye Chama Cha Mapinduzi,’’ alisema Bugota.
Katika hatua nyingine, Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi Tabora, Bi. Anna Mbasha aliwakumbusha viongozi hao wanatakiwa kufanya maamuzi kwa kuzingati sheria, kanuni na taratibu ambalo ni takwa la msingi katika uwajibikaji wa pamoja.
Alisema wanatakiwa kuwa na uwajibikaji wa pamoja wa kimaadili kwa kufanya kilichokuwa sahihi wakati wowote hata kama hakuna mtu yoyote hususan viongozi wanaomwangalia katika utekelezaji wa majukumu yake.
‘’Tunaposema uwajibikaji wa pamoja tunahimiza twende pamoja kwa lengo la kuhakikisha shughuli za serikali zinatekelezwa na kuiona thamani ya fedha na kuepuka kulaumiana na kunyoosheana vidole,’’ alisistiza.
Kwa upande wa Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo, Bi. Shani Mangesho alimpongeza Rais Dk. Samia kwa namna ambavyo ameendelea kuiweka Tanzania katika hali ya usalama muda wote.
‘’Kwa hakika nchi ipo shwari kwa sababu leo hii tukiangalia wenzetu wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo wanavyokimbia kwa kweli inatia huruma lakini Tanzania tunajidai, tunatembea kifua mbele na kufanya kazi zetu ni jambo la kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia,’’ alisema.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sauda Mtondoo aliwataka Madiwani kuendelea kuwa karibu na wananchi kuwaeleza yale mambo ambayo serikali imetekeleza ikiwemo ambayo inatarajia kuyafanya kwa lengo la kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Selwa Abdalla Hamid alisema amepokea yote yaliyoelekezwa katika ofisi yake kwa lengo la kuyafanyia kazi.
Aidha, aliahidi kuhakikisha Wataalamu wanaingiza katika bajeti inayoandaliwa hivi sasa ya mwaka wa fedha 2025 hadi 2026 suala la kununua vishikwambi vitakavyokuwa vikitumiwa na Madiwani katika vikao vijavyo.
==== //// ==== //// ==== //// =====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa