MSIMAMIZI wa Uchaguzi wa Majimbo ya Igunga na Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora, Ndug. Hamisi H. Hamisi amesema wapiga kura 273,076 wanatarajia kupiga kura ifikapo Oktoba 29, mwaka huu katika majimbo hayo.
Ndug. Hamisi ameeleza hayo leo jumapili Oktoba 26, 2025 katika ofisi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliyopo katika wilaya hiyo mjini Igunga.
Kwa mujibu wa kifungu cha 69, (1) cha sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Ndug. Hamisi amewatangazia wananchi waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la wapiga kura la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuwa uchaguzi utafanyika siku ya Jumatano Oktoba 29 mwaka huu.
Ameeleza kuwa vituo vilivyotumika kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura ndio vitatumika kupiga kura.
Ameweka wazi kuwa vituo vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa 10 jioni huku kwa upande wa vituo vilivyoko Magereza vitafunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa tisa alaasiri.
"Nitumie fursa hii kuwaomba na kuwakaribisha wananchi wote wa majimbo ya Igunga na Manonga kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 29, Oktoba 2025 kwa lengo la kupiga kura," ametoa wito.
Aidha, ameeleza katika majimbo hayo kuna jumla ya vituo vya kupigia kura 728 ambapo vyote vipo tayari kuhakikisha zoezi hilo linatimia kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, amedokeza kuwa wanaendelea na zoezi la kuwahamasisha wananchi kwa njia ya matangazo, matamasha na michezo kwa lengo la kuwakumbusha na kuwahimiza wananchi kujitokeza kupiga kura.
Amewahakikishia wananchi kuelekea Oktoba 29, mwaka huu wamejipanga vema kufanikisha zoezi la uchaguzi kwa ufanisi.
"Tumeishapokea vifaa vyote wa uchaguzi na vipo tayari na zoezi la kusambaza katika vituo limekamilika," amethibitisha.
Tanzania hufanya uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano, hivyo zikiwa zimebaki siku takribani tatu wananchi watapiga kura kutimiza haki yao ya kikatiba.
===================/



Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa