MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Mhe. Lucas Bugota amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameleta fedha nyingi ambazo zimekua zikitekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za maji, afya, elimu, umeme na miundombinu.
Mhe. Bugota aliyasema hayo Jumatano Januari 29, 2025 wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Meneja wa Wilaya – TARURA, Aswile Mwasaga aliishukuru serikali kwa kuwapa nyongeza ya bajeti kwa lengo la kuboresha miundombinu ya barabara.
Aidha, aliweka wazi kuwa Igunga inakilometa 19.185 za barabara za kiwango cha lami, kilometa 376.39 barabara za kiwango cha changarawe, kilometa 819.079 kiwango cha udongo, Madaraja 29, Drift na Makalvati 371.
Katika hatua nyingine, Taarifa ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia Meneja wa Wilaya hiyo, Mhandisi Raphael Ambonisye ilidokeza kuwa vijiji 119 vimefikiwa na umeme.
Iliweka wazi kuwa inatekeleza mradi unaofadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupeleka umeme kwenye vitongoji 3,060 huku ikikadiriwa kutumia takribani sh. bilioni 2.691 ambapo Mkandarasi amekwisha kamilisha kazi ya kukagua (Survey) na anaendelea na kuhamasisha (Mobilazation) na Procurement (Manunuzi) kwa lengo la kuanza kazi ya kujenga laini.
Kwa upande wa Taarifa ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini (IGUWASA) kupitia Kaimu Mkurugenzi Mtendaji – IGUWASA, Mhandisi Bakari Mohamed ilibainisha kuwa huduma ya kupata maji ni nzuri na inakidhi katika eneo lote ambalo IGUWASA inahudumia.
Pia, ilieleza kuwa Mtandao wa kusambaza maji umeongezeka katika maeneo ya pembezoni mwa mji kutoka Bunjiri kuelekea kijiji cha Majengo kilometa 3.5, kufungua vitua vingine kijiji cha Mwalala kupitia upanuzi wa Mtandao wa maji kilometa 1.07 na kupanua huduma ya upatikanaji wa maji kilometa 4.8 kijiji cha Ikulamawe.
Nayo Taarifa ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kupitia Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya hiyo, Mhandisi Johnbosco Basabwa ilieleza kuwa inatekeleza mradi wa uchimbaji wa visima 10 katika vijiji vya Ncheli, Kazima, Igumo, Igondela, Igoweko, Kityelo, Imenya, Mgazi, Nguvumoja na Ibole kwa gharama ya sh. Milioni 600.
Aidha, ilitaja mradi mwingine ni upanuzi wa mradi wa maji ya ziwa Victoria kutoka Ziba kwenda Nkinga awamu ya pili unagharimu sh. bilioni 2.114 na upanuzi wa mradi wa maji ya ziwa Victoria kutoka Nkinga kwenda Simbo unaogharimu sh. Bilioni 1.032.
===== //// ==== ///// ====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa