Siku ya mazingira duniani huadhimishwa tarehe 05 mwezi Juni kila mwaka. Katika Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini, Maadhimisho haya yalianza tarehe 29 mwezi Mei na leo tarehe 05 mwezi Juni ndiyo kilele chake. Kilele cha sherehe za Maadhimisho haya kitaifa zinafanyika Jijini Dodoma na kimkoa ni katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Kwa mwaka huu maadhimisho ya kiwilaya yamefanyika katika kijiji cha Bukoko.
Shughuli mbalimbali zilitekelezwa katika kipindi cha maadhimisho haya kama vile kufanya usafi wa mazingira, upandaji wa miti pamoja na utoaji elimu ya kuhifadhi na kutunza mazingira.
Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya kitaifa ni “Urejeshwaji wa Ardhi, na Ustahimilivu wa hali ya Jangwa na Ukame”. Kaulimbiu ya mwaka huu inatukumbusha kuwa Ardhi yetu imeharibiwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu na kwa sasa inatulazimu kurejesha uoto wa asili ili kuweza kustahimili hali ya Jangwa na Ukame inayosababishwa na Mabadiliko ya Tabia ya nchi.
Tunapoadhimisha siku hii ya mazingira duniani ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo;
1. Usafi usimamiwe kikamilifu na wananchi wote bila jukumu hilo kuziachia mamlaka za serikali pekee au kusubiri matamko ya viongozi wa juu. Pia ni vyema kuacha kabisa mazoea mabaya ya kutupa takataka hovyo ili kudumisha usafi wa maeneo yetu. Mfano unakuta mwananchi baada ya kunywa maji au juisi chupa inatupwa popote ama baada ya kula biskuti au karanga vifungashio vinaachwa hapo hapo, hii siyo sawa.
2. Kuacha kujichukulia sheria mkononi na kukata miti bila kufuata utaratibu. Kila mwananchi anayehitaji kukata miti kwa ajili ya kuni, kuchoma mkaa, kupasua mbao n.k ni lazima apate kibali halali kutoka mamlaka za serikali.
3. Kuepuka kilimo cha kuhamahama kwani kinachochea ukataji hovyo wa miti wakati wa kusafisha mashamba. Kilimo hiki huharibu uoto wa asili, kupoteza viumbe na hatimaye kusababisha jangwa. Badala yakenawashauri muwatumie maafisa ugani ipasavyo ili kupata elimu na ushauri wa kitaalamu juu ya nini cha kufanya katika Ardhi inapopungukiwa na rutuba.
4. Kupanda na kutunza miti kuna faida nyingi katika maisha yetu ya kila siku. Katika miti ndipo tunapata kuni, mkaa, mbao, nguzo, magogo, hewa safi, vivuli, matunda na dawa mbalimbali za asili. Faida zingine ni kuongeza thamani ya Ardhi, kuvuta mvua, kutuliza fukuto la joto na kufyonza hewa ukaa.
Halmashauri ya Wilaya ya Igunga inayo sheria ndogo ya Usafi na Mazingira ya Mwaka 2021 ambayo inatutaka kila kaya kupanda miti isiyopungua mitano kila mwaka. Kuwa na sheria hii pekee yake bila utashi ni vigumu kufanikiwa. Hivyo nawaombeni wananchi wote tupende sana kutunza mazingira yetu yanayotuzunguka kwa kupanda miti kwa wingi.
5. Maeneo ya vyanzo vya maji yanatambulika na kulindwa na sheria mbalimbali za Nchi. Ikumbukwe kuwa sheria ya Mazingira inaelekeza kuacha kufanya shughuli yeyote katika umbali wa mita 60 kutoka kwenye eneo la chanzo cha maji au kingo za mito. Hivyo nawataka wataalamu na viongozi wote mnaohusika kuanza kuchukua hatua kwa wananchi wote wanaofanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji hususani kwenye kingo za mito.
6. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan akiwa Dubai kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi mnamo tarehe 02/12/2023 alizindua mradi wa nishati safi ya kupikia kwa wanawake wa Afrika. Mradi huu ni wa miaka 10 ambao unakusudia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia hadi kufikia asilimia 80 ya watanzania wote. Hivyo nawaombeni taratibu tuanze kuondokana matumizi ya nishati chafuzi kwa maana ya kuni na mkaa na kujielekeza kwenye matumizi ya nishati safi.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa