MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Frof. Davis Mwamfupe amewakumbusha Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora kuendelea kufahamu kuwa maendeleo yatapatikana kwa kudumisha ushirikiano.
Prof. Mwamfupe ameyasema hayo katika Ukumbi wa Mikutano wa Manisapa ya Zamani jijini Dodoma wakati Madiwani na Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga walipofanya ziara ya kuangalia utekelezaji wa miradi ya Halmashauri ya jiji hilo.
Amesema Halmashauri zitaendelea kustawi pale watakapokuwa na ushirikiano madhubuti kati ya Madiwani na Wataalamu huku wakifahamu wao ni jeshi kubwa, hivyo wawe na maamuzi makubwa yanayotokana na kuaminiana kwao.
Ameeleza kuwa wanahitajika kuwa na uthubutu wa kufanya maamuzi wa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wao, hivyo Halmashauri zao zinahitaji kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha vilivyopo kupata fedha zinazowezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Lucas Bugota amempongeza Mstahiki Meya huyo kwa namna alivyowaelimisha, hivyo wamejifunza mengi.
Amesema licha yakuwa mapato ya Igunga ni madogo ukilinganisha na yale ya Halmashauri ya jiji hilo lakini ni lazima wafanye jambo kupitia asilimia 40 zinazotokana na mapato ya ndani.
‘’Tumeyachukua na kuyazingatia yote tuliojifunza kwa manufaa ya wananchi wetu na kuendelea kumuunga mkono Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mambo anayoyafanya,’’ amesisitiza.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Bi, Selwa Abdalla Hamid amewashukuru viongozi wa Halmashauri ya Jiji hilo kwa sababu walipokelewa vema, hivyo wamejifunza mengi hususan ikizingatiwa kuwa elimu haina mwisho.
‘’ Ninakushukuru Mstahiki Meya kwa kutupokea, tumejifunza mengi ikiwemo miradi mikubwa yenye thamani ambayo mmeitekeleza, imetupa ari kweli na tutaenda kutekeleza kwa uwezo wa Halmashauri yetu,’’ amesema.
Katika Hatua nyingine, amewakumbusha Wataalamu na Madiwani hao kuwa ukusanyaji wa mapato ni vita kwa sababu hakuna mtu ambae anafanya biashara halafu anataka kutoa ushuru au kopdi kwa utashi, hivyo waendelee kutoa elimu ya kuhamasisha walipie mapato hayo.
‘’Ndugu zangu, kupata maendeleo ni lazima ushuru ukusanywe katika niia zilizohalali, hivyo tukawe mabalozi wazuri wa kufikisha ujumbe wa kulipa ushuru kihalali tena bila ya kushurutishwa,” amebainisha.
Ameeleza kuwa nilazima wapate mambo mazuri kwa kutanguliza uzalendo mbele jambo ambalo litawawezesha kukubaliana kuwa tayari kulipa mapato ambayo ndiyo yanayoleta maendeleo ya Halmashauri.
Naye Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Grace Mwema ameweka wazi wamejifunza namna bora ya matumizi ya fedha za ndani hususan katika kuibua miradi na kuweza kuisimamia.
Aidha, ameipongeza serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuisaidia Halmashauri ya jiji hilo huku akiiomba kuendelea kutupia jicho na Halmashauri ya Igunga.
‘’Hakika sisi Wataalamu na Waheshimiwa Madiwani tumeondoka tukiwa na motisha na morari ya kazi na tunaahidi kwenda yatekeleza tuliyojifunja, hivyo Halmashauri ya wilaya Igunga inakwenda kuibuka mshindi katika kutekeleza na kusimamia miradi,’’ amedokeza.
====////====////====
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa