WANUFAIKA wa mikopo itokanayo na asilimia 10 wameendelea kumshukuru na kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuirejesha tena kwa utaratibu ambao umetajwa kuwa na ufanisi na wenye uhakika wa kufuatilia wanufaika hao kwa lengo la kuhakakikisha wanarejesha fedha hizo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuvipatia mikopo ya sh milioni 107.5 Vikundi saba vilivyokidhi vigezo katika robo hii ya mwaka wa fedha katika ukumbi wa Maxwel, Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Sauda Mtondoo amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuendelea kuwainua wananchi kiuchumi.
‘’Kipekee nimpongeze na kumshukru Rais wetu Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira ya dhati ya kuwainua watanzania wakiwemo wajasiriamali kiuchumi,’’ ameshukuru na kuongeza kuwa:
“Hakika kwa kutumia muongozo mpya wanajihakikishia kikundi kinachokopeshwa kitakua na uwezo wa kufanya biashara na kurejesha fedha zilizokopeshwa.”
Aidha, amewataka Wataalamu waendelee kutoa elimu kwa wananchi mambo gani ya msingi wanapaswa kuyazingatia kwa lengo la kuwa na sifa ya kukopesheka kwa sababu dhamira ya Rais Dk. Samia ni kuona fedha inayotengwa inakwenda kwa watu waliokidhi vigezo vya kupata mkopo.
Ameeleza hatua hiyo itasaidia Jamii kufanya shughuli za kujiongezea kipato na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja jambo ambalo litachangia kukuza uchumi wa Halmashauri, Mkoa hadi Taifa.
Hata hivyo, amewaomba wananchi ambao wamepata mkopo kuwa waadilifu, waaminifu na kuwa mfano wa kurejesha fedha walioikopo kwa mujibu wa mikataba waliyokubaliana kwa lengo la kuwakopesha wananchi wengine watakaokua na sifa kama wao.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Selwa Abdalla Hamid amewataka wananchi ambao hawajaunda vikundi kujifunza kwa waliokwishaunda kwa sababu fedha za kuwakopesha zipo na zinahitajika zifike kwa vinaja, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu ambao ni wajasiriamali.
Pia, amewafahamisha kuwa fedha hizo ni mkopo ambao sharti lake ni kurudisha kwa lengo la kuhakikisha inawanufaisha wananchi wengine wenye sifa.
‘’Tukiitumia mikopo hii vizuri itawafaidisha wananchi wengi na kuinuka kiuchumi, hivyo sisi halmashauri tutaendelea kutenga fedha na kutimiza malengo ya Rais Dk. Samia ya kuwainua wananchi kiuchumi na wapate kipato chao cha halali,”amesisitiza.
Pia, amewatoa hofu wananchi ambao wamekosa mikopo awamu hii wasikate tamaa kwa sababu fedha ipo ya kutosha, hivyo watimize vigezo, masharti, kanuni na taratibu watapata tu.
‘’ Hata kama utakosa mara 10 rudi na kajirekebishe tena kwa sababu ukiwa na nia huenda mara ya 11 utapata mkopo, fedha zipo na tunatamani mfuko wetu ubakie ziro na fedha zote zije kwenu,’’ ameweka wazi.
Awali akiwasilisha taarifa fupi mbele ya Mkuu huyo wa wilaya, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, John Tesha amesema utoaji wa mikopo ni endelevu na fedha inayotolewa katika robo husika ikibaki itahamishiwa karika robo inayofuata huku akionya kuwa kikundi kitakachochindwa kupeleka marejesho kwa wakati hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Naye mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo, Daniel Kulyama ametoa wito kwa wananchi wengine waombe mikopo hiyo iwainue katika biashara zao na kukua kiuchumi.
‘’Ninamiaka zaidi ya mitatu ninafuatilia mkopo lakini awamu hii nimepata fedha za Halmashauri kupitia kundi la walemavu, hivyo ninawahamasisha wenzagu ambao wanajishughulisha na ujasiriamali waombe watapata na kuinua mitaji yao ikiwemo kukuza uchumi,” amesema.
=======
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa