MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkaoni Tabora, Bi Selwa Abdalla Hamid amewakumbusha wananchi umuhimu wa kutunza afya zao na kutakiwa kuwa na tabia za kutembelea Hospitali kwa sababu watagundua umuhimu wa hilo.
Bi, Selwa ameyasema hayo Jumapili Desemba 01, 2024 katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika katika Kata ya Ibologero kijiji cha Ibologero mjini hapa.
“Ndugu wananchi niwasihi tuendelee kujilinda sisi na ndugu au familia zetu dhidi ya gonjwa la UKIMWI,’’ amesema.
Katika hatua nyingine, Bi. selwa amewataka watu waliokwisha ambukizwa gonjwa hilo kutokua na tabia ya kuwaambukiza wengine kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kuangamiza Taifa na kutenda dhambi kwa kumuhujumu mtu kwa makusudi.
Amesema ni vyema kila mmoja akawa na tabia ya kwenda kupima kwa lengo la kuelewa hali yake ya maambukizi ikoje aidha ameambukizwa au la na wasiogope kufanya hivyo kwa kuwa upo usiri wa kutunza taarifa zao.
Ameweka wazi kuwa katika wilaya hii kunawananchi takribani 546,204 ambapo katika hao watu 938 wamekwisha ambukizwa huku asilimia 71 wanajitambua na asilimia 29 hawajitambui jambo ambalo ni hatari.
Amesema njia sahihi ina maana pana ikiwemo wale waliofika umri waendelee kubakika katika ndoa zao huku akiwakumbusha tabia ya kuwa na mchepuko sio njia sahihi.
Aidha, amewahamasisha wananchi kuwa na tabia ya kupanda miti nakuacha kukata miti huku akiahidi kutoa miti kwa watu ambao watakua wamejipanga kupanda miti.
“Nitoe wito ndugu zangu katika maeneo yenu mpande miti na watakao kosa miche mimi nitawasaidia kwa lengo la kuhakikisha Igunga yetu inabaki kuwa ya kijani na kuwaachia vizazi vijavyo mazingira salama,” amessistiza.
Akizungumza katika Hafla hiyo Afisa Tarafa ya Manonga ambae ni Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Martha Tevel amewashukuru Wadau wa Maendeleo ambao wamekuwa wakishirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokomeza janga la UKIMWI.
Awali akiwasilisha taarifa ya hali halisi ya maambukizi ya UKIMWI Mratibu wa UKIMWI ngazi ya jamii wa wilaya hiyo, Devotha Macheku amefafanua maana ya kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Chagua Njia Sahihi Tokomeza UKIMWI” kuwa ni mtu akipima na kugundulika kuwa amepata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ajiunge na huduma ya matunzo na tiba.
Hatimiliki@2017Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Haki zote zimehifadhiwa